Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu, amewasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu marekebisho ya mfumo wa kodi, ada na tozo kwa mwaka wa fedha 2025/26, kwa lengo la kuongeza mapato ya Serikali, kuboresha ukusanyaji na usimamizi wa mapato pamoja na kudhibiti upotevu wa fedha za umma.
Akizungumza leo Bungeni Dodoma 12 Juni 2025, Waziri Nchemba amesema maboresho hayo yamezingatia mabadiliko ya sera za kiuchumi duniani, hasa kutoka Marekani, na yataimarisha mfumo wa kodi kuwa tulivu na wa kutabirika ili kuchochea uzalishaji mali katika sekta muhimu za uchumi kama viwanda, madini, kilimo, ufugaji, nishati, usafirishaji, elimu na afya.
Aidha, Waziri ameeleza kuwa marekebisho haya yanatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni 4.26, na yatahusu marekebisho katika sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sheria ya Kodi ya Mapato, Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sheria ya Madini, Sheria ya Bima, pamoja na sheria nyingine 25 zinazohusiana na ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa biashara.
Miongoni mwa mabadiliko yaliyopendekezwa ni pamoja na kusamehe kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye viuatilifu maalum ili kuwasaidia wakulima kupata dawa za kuua wadudu kwa bei nafuu, na kusamehe VAT kwenye ununuzi wa bima mtawanyo (reinsurance) ili kukuza ushindani katika sekta ya bima na kuhamasisha ukuaji wake.
Aidha, Waziri Nchemba amesisitiza umuhimu wa kuendeleza mfumo wa kodi ambao unakuza sekta za kimkakati na kusaidia kukuza uchumi wa taifa, kuongeza ajira na kupunguza umasikini kwa wananchi.
Maboresho hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuongeza mapato ya ndani, kupunguza utegemezi wa fedha za nje, na kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanafanikiwa kwa ufanisi.