Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Serikali imetoa onyo kwa waajiri wote nchini wanaowatumia watoto kama nguvu kazi kwa namna yoyote ile, huku ikiweka wazi kuwa ni marufuku kuwatweza watoto kwa kuwavunja haki, heshima na utu wao.

Kauli hiyo imetolewa leo Juni 12,2025 ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji Watoto, ambapo Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, amesema kuwa ni lazima taifa lizinduke na kuwalea watoto katika mazingira salama na ya heshima.

Amesema Watoto ni kizazi kinachopaswa kulelewa kwa malezi bora na kwamba Serikali haitavumilia kuona mtoto anafanyishwa kazi hatarishi au kuingizwa kwenye ajira kwa namna yoyote ile.

Amesema katika kufanikisha hilo tayari serikaki imeongeza magari ya ukaguzi wa kazi za watoto ili kuongeza ufanisi.

Kaimu Mkurugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki Groly Emmanuel amesema bado watoto milioni 160 duniani wanatumikishwa kwenye kazi mbalimbali, huku wengi wakihusishwa na kazi hatarishi.

Amesema 70% ya watoto wanaotumikishwa duniani hufanya kazi kwenye sekta ya kilimo na kufafanua kuwa Kusini mwa Jangwa la Sahara imepunguza kiwango cha utumikishaji watoto kwa asilimia 10 tangu mwaka 2020.

“Asilimia 24.9 ya watoto duniani wako kwenye kazi mbaya zaidi zinazohatarisha maisha yao, ” Amesema.

Ameeeza kuwa licha ya hatua zilizopigwa duniani, bado mtoto wa kike anaendelea kuathirika zaidi, hasa katika kazi za ndani ambazo mara nyingi hufanywa kwa siri na kwa mazingira yasiyo rafiki kwa mtoto.

Kutokana na hali hiyo amesema ILO limetoa mapendekezo kwa Nchi Wanachama kukuza ajira zenye staha kwa wazazi ili kuondoa utegemezi wa kipato kupitia watoto,Kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii na Kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ajira kwa watoto.

Mapendekezo mengine ni Kuweka na kutekeleza sheria kali dhidi ya waajiri wanaotumikisha watoto na Kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, jamii na mashirika ya kiraia.

Kaimu Mkurugenzi huyo amesema ILO imeorodhesha haki muhimu zinazokiukwa pale mtoto anapofanyishwa kazi, zikiwemo haki ya kupata elimu bora,haki ya afya na ustawi,kucheza na kupumzika,kulindwa dhidi ya kazi hatarishi na kukua katika mazingira salama na yenye staha.

Kwa upande wake Kamishna wa Kazi, Susan K. Mkangwa, amesema Idara ya Kazi imepanga kufanya kaguzi maalum katika mashamba, migodini na maeneo ya kazi kote nchini ili kubaini watoto wanaotumikishwa na kuchukua hatua kali kwa waajiri watakaobainika.

“Tutahamasisha jamii kwa kampeni za elimu juu ya madhara ya utumikishwaji watoto,lengo ni kuondoa kabisa aina zote za ajira kwa watoto,” amesema Kamishna Mkangwa.

Amesema Tanzania pia imeridhia mikataba mikubwa miwili ya kimataifa ya ILO Na. 138: Unaoweka umri wa chini wa ajira na Mkataba Na. 182: Unapiga marufuku aina mbaya zaidi za ajira kwa watoto ili kumlinda mtoto na kumuacha akiwa salama.