Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Serikali imeandaa hati 7,000, kupima na kutambua zaidi ya viwanja 18,000, pamoja na kugawa hati miliki kwa wananchi wa mitaa ya Pangani, Kidimu na Lumumba katika Kata ya Pangani, Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, alizindua rasmi zoezi la ugawaji wa hati kwa wakazi 186 wa mitaa hiyo Septemba 3, 2025, inayolenga kupunguza ama kumaliza migogoro ya ardhi, hasa migogoro ya mipaka.

“Moja ya changamoto kubwa zilizokuwepo katika Kata ya Pangani ilikuwa ni migogoro ya ardhi, kwa hatua hii wataalamu wa ardhi waendelee kuweka kambi katika eneo hili ili kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi,” alisema Simon.
Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kulipia ardhi zao ili waweze kumiliki kihalali na kupatiwa hati miliki, “
“Huu ni muendelezo wa kuhakikisha Wilaya ya Kibaha inapangwa, inapimwa, na kila mwananchi anapata hati miliki,” aliongeza.
Simon pia alieleza mafanikio yaliyopatikana chini ya Serikali ya Awamu ya Sita ni pamoja na kutatua changamoto ya fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa barabara ya lami hadi Baobab, utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji ambao mkandarasi tayari yupo eneo la mradi, upimaji wa viwanja, utoaji wa hati miliki, ujenzi wa zahanati ya Pangani na uanzishwaji wa shule mpya ya Mtakuja.

Aliwataka wananchi ambao bado hawajalipwa fidia zao kufika ofisini kwake Jumatano ijayo kwa ajili ya kushughulikiwa.
Kwa upande wake, Msajili Msaidizi wa Hati Mkoa wa Pwani, Burton Rutta, alisema kuwa hadi sasa wamefanikiwa kupima asilimia 80 ya maeneo yaliyokusudiwa.
Rutta alieleza ,mbali na ugawaji wa hati, wameendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa hati miliki, faida za kumiliki ardhi kihalali, pamoja na umuhimu wa kulipa kodi.

“Serikali ya Awamu ya Sita imerahisisha mchakato wa upatikanaji wa hati kwa kupunguza gharama zake kwa asilimia 50, ikiwemo ada za maombi ya umiliki wa ardhi,” alifafanua Rutta.
Baadhi ya wakazi wa Kidimu, akiwemo Esther Chacha, waliishukuru serikali kwa kuwapatia hati na kutekeleza zoezi la upimaji ardhi, wakisema kuwa hatua hiyo itasaidia kumaliza migogoro ya ardhi ambayo ilikuwa imekithiri katika kata hiyo.


