Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali imetakiwa kufanya tathmini ya hali ya kifedha ya Asasi za Kiraia (NGOs) kufuatia kufutwa kwa misaada kutoka serikali ya Marekani na baadhi ya nchi nyingine zilizoanza mchakato wa mabadiliko ya utoaji wa misaada hiyo.
Wito huo umetolewa leo Bungeni na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Neema Lugangira anayewakilisha kundi la NGOs, wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
“Ni muhimu serikali kupitia Wizara hii ifanye tathmini ya hali ya kifedha ya NGOs baada ya misaada mingi kutoka Marekani na nchi nyingine kufutwa. Tunahitaji kujua hali halisi ili sekta hii muhimu isiathirike zaidi,” alisema Lugangira.
Aidha, alikumbusha kuwa mwaka 2023 Rais Samia Suluhu Hassan alielekeza serikali kuharakisha uanzishwaji wa mfuko wa pamoja wa NGOs (NGOs Basket Fund).
“Naomba Waziri atueleze, mfuko huu umefikia hatua gani hasa ikizingatiwa hali ya sasa ya kiuchumi na kupungua kwa misaada ya kimataifa,” alihoji.
Katika hoja nyingine, Lugangira aliiomba serikali kuhakikisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inazitambua na kuzipambanua NGOs na taasisi za kibiashara.
“Ni vyema TRA watofautishe kati ya NGO na biashara. Hatuwezi kuendelea kuzikamata NGOs kana kwamba ni wafanyabiashara,” alisema.
Katika mchango wake, Lugangira pia ameeleza changamoto ya NGOs kutotambulika katika mfumo wa ulinzi binafsi nchini, hali inayozisababisha kulazimika kujisajili kama taasisi za biashara ili kupata huduma hizo. Ameiomba serikali kufanya marekebisho ya sheria ili kutambua rasmi NGOs kama kundi maalum linalostahili msamaha wa malipo ya usajili kwenye mifumo ya ulinzi binafsi.
Amewashukuru wadau wa NGOs kwa ushirikiano waliompatia katika kipindi chote cha uwakilishi wake, na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na weledi kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Aidha, amewatoa hofu wakazi wa Bukoba kwa kuwahakikishia kuwa ataendelea kushirikiana nao katika kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi, huku akionesha matumaini ya kuendelea kuaminiwa na uongozi wa UWT katika ngazi ya kitaifa ili kazi iendelee.
