Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Serikali imeeleza kusikitishwa kwake na azimio la Bunge la Ulaya la baadhi ya watendaji wa kimataifa kutoa maamuzi kwa kuzingatia taarifa zisizo kamili.
Imesema imezingatia azimio lililopitishwa na Bunge la Ulaya tarehe 8 Mei 2025 kuhusu taratibu za kisheria zinazoendelea nchini Tanzania.
”Wakati Tanzania inaheshimu uhuru wa kitaasisi wa Bunge la Ulaya na kuthamini ushirikiano wake na Umoja wa Ulaya, inaona ni muhimu kufafanua baadhi ya mambo muhimu na kusisitiza dhamira yake ya muda mrefu ya maadili ya kidemokrasia, utawala bora na utawala wa sheria”. Wizara ya mambo ya nje ya Tanzania imeeleza katika taarifa yake.
Serikali imesema kuwa tangu Machi 2021 imefuata mageuzi mapana ya kisiasa na kisheria chini ya falsafa ya 4Rs- Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi Upya.
Marekebisho haya yameleta matokeo yanayoonekana, ikiwa ni pamoja na kurejeshwa kwa uhuru wa kisiasa, upanuzi wa uhuru wa kiraia, kuimarishwa kwa uhuru wa vyombo vya habari, na kupitishwa kwa sheria mpya za uchaguzi Machi 2024, ambayo ilisababisha kuanzishwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Imesema Tanzania ni nchi huru yenye katiba yake na inaongozwa na utawala wa sheria na kuwa masuala yote ya kisheria yanashughulikiwa kwa uhuru na Mahakama ikiwa ni moja ya mihimili ya nchi, kwa kuzingatia sheria za nchi na kwa kuzingatia viwango na taratibu bora za kimataifa, pale ambapo Serikali haiingilii mashauri ya kimahakama.
“Kwa hiyo, kauli zinazoashiria au kuhimiza uingiliaji kati wa watendaji katika kesi zinazoendelea si tu kwamba hazifai, bali pia ni kinyume na kanuni ya uhuru wa kimahakama kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Tanzania na inavyotetewa na Umoja wa Ulaya. Ilieleza katika taarifa yake”.
