Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kulinda bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (JNHPP) ikiwemo kutekeleza sheria ya kudhibiti shughuli za kibinadamu.

Kauli hiyo ameitoa June 12,2025 bungeni wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Donge Soud Mohamed Jumah (CCM) alitaka kujua mkakati wa serikali katika kuimarisha uhifadhi wa mazingira ya Mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere ili kuhakikisha uendelevu wa mradi.

Akijibu,Khamais amesema wananchi wanashirikishwa vya kutosha katika kupewa elimu ya utunzaji wa maeneo yote yanayozunguka bwawa hilo na kwenye vyanzo vyote vya maji yanayoelekea kwenye bwawa hihlo ikiwemo kutokata miti ambalo ni kosa kisheria lakini pia kuwahamasisha kupanda miti ambalo ni jambo la kisheria.

“Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere litasaidia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ya umeme hali itakayosaidia kutunza misitu katika eneo hilo,”alisema Khamis

Pia amesema serikali inaendelea kutoa elimu ya mazingira, kusimamia utekelezaji wa Muongozo wa Taifa wa Matumizi endelevu ya Ardhi Eneo la Hifadhi ya Mita Sitini (60) kutoka kwenye vyanzo vya maji pamoja na kuunda kamati za mazingira kwa ajili ya kudhibiti uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya maji.