Na OR-TAMISEMI, Iringa

NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinyijuma amesema Serikali imetenga Shilingi Bilioni 11 kwa ajili ya kutekeleza mpango wa kuboresha miundombinu ya michezo katika shule 10, kati ya shule 56 maalum za michezo zilizopo nchini.

Akizungumza Juni 20, 2025, wakati wa ufunguzi wa Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) yanayofanyika mkoani Iringa, Mwinyijuma amesema lengo la mpango huo ni kuweka mazingira rafiki kwa michezo na sanaa shuleni, ili kuwaandaa wanamichezo na wataalamu wenye uwezo wa kushindana katika ngazi ya kimataifa.

Aidha, alisema Serikali imetenga Shilingi Bilioni 32 kwa ajili ya kuimarisha Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, ambapo ujenzi wa Akademia ya Michezo ya Kitaifa unaendelea.

Alieleza kuwa kukamilika kwa akademia hiyo kutawawezesha wanamichezo wenye vipaji kupata mafunzo ya kitaalamu na kukuza uwezo wao.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo alisema Serikali imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Michezo kwa lengo la kusaidia shughuli mbalimbali za michezo nchini, ikiwa ni pamoja na kuwezesha wanamichezo na taasisi zinazojihusisha na sekta hiyo kufanikisha malengo yao.

Vilevile, alisema Serikali ina mpango wa kuanzisha Wakala wa Usimamizi wa Miundombinu ya Michezo nchini (Sports Infrastructure Management Agency – SIMA), pamoja na kufufua Mfuko wa Sanaa na Utamaduni Tanzania, ambao utatoa mikopo yenye riba nafuu kwa wasanii na taasisi zinazojihusisha na sekta ya sanaa na utamaduni.