Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imewataka Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi nchini kuhakikisha jamii inawatambua na kuwatumia katika masuala ya majenzi ili waweze kuwa na makazi bora
Pia imetoa maagizo manne kwa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), ikiwemo kufanya tafiti za kina ili kuwatambua wahitimu wa taaluma hizo na kuhakikisha wanasajiliwa mapema kwa ajili ya kutoa huduma kwa jamii.

Akuzungumza mara baada ya kufungua semina elekezi kwa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi Dar es Salaam jana Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Dkt. Charles Msonde alisema watanzania wengi wamekuwa na mawazo hasi kwa kudhani kuwa hawana umuhimu wa kuwatumia wataalamu katika Majenzi na hivyo kusababisha baadhi yao kutokuwa na makazi bora
Akizungumzia kuhusu maagizo kwa bodi ya AQRB Dkt Msonde alisema huduma zinazotolewa na wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi nchinu ni muhimu kwa maendeleo endelevu, hivyo ni wajibu wa bodi kuhakikisha wahitimu wanatambuliwa mapema na kuingizwa kwenye mfumo wa kazi rasmi.
“Ndani ya vyuo vyetu kuna wahitimu wengi lakini hawajui nini cha kufanya baada ya kuhitimu bodi fanyeni tafiti za kina ili kuwatambua na kuwasajili hata kwa mfumo wa mafunzo kwa vitendo (internship). Hii itawasaidia kupata uzoefu wa kazi na kujiamini,” alisema Dkt Msonde.

Aliyataja maagizo mengine Kwa bodi hiyo kuwa ni pamoja na kuweka mazingira rafiki kwa wataalamu hao kupata fursa katika soko la ushindani, ikiwa ni pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) yatakayosaidia kuuza ubunifu wao kwa mataifa mengine.
Dkt. Msonde aliwaagiza kuhakikisha wataalamu waliopitishwa na bodi ni wale wenye weledi na uwezo wa kusimamia miradi kwa ubora hata pale wakandarasi wakuu wanapoondoka wao wabaki wakiwa vinara katika kuendeleza miradi hiyo.

Aisha aliagiza kutafutwa vyanzo mbadala vya fedha ili kuhakikisha mafunzo yanayotolewa kwa wataalamu hao yanakuwa endelevu na yenye tija katika kukuza taaluma zao.
Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa bodi hiyo, Mbunifu Majengo Daniel Matondo, alisema AQRB ilianzishwa rasmi mwaka 2010 kwa lengo la kusimamia, kudhibiti weledi, maadili, na ubora wa huduma zinazotolewa na wataalamu wa sekta hiyo nchini.

Alisema tangu utekelezaji wa majukumu ya bodi uanze mwaka 1998, mafanikio makubwa yamepatikana hadi kufikia Juni 2025, jumla ya wataalamu 1,707 na makampuni 491 wamesajiliwa na bodi hiyo, ikilinganishwa na wataalamu 188 na makampuni 53 mwaka 1998.
“Ni muhimu wataalamu wetu washirikishwe kikamilifu tangu hatua za awali za upangaji wa miradi hadi utekelezaji wake. Hii itasaidia kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa rafiki kwa mazingira na inaendana na changamoto za sasa kama mafuriko, msongamano wa magari na ongezeko la watu mijini,” alisisitiza Mbunifu Majengo Matondo.
Alieleza kuwa bodi imekuwa ikiendesha Programu ya Mafunzo ya Vitendo kwa wahitimu, ambapo jumla ya wahitimu 1,223 wamenufaika tayari, na wengine 283 wakiendelea na mafunzo hayo.
Kwa mujibu wa Mbunifu Majengo Matondo, programu hiyo inalenga kuwaandaa wahitimu kwa soko la ajira na kuwaongezea uwezo wa vitendo kabla ya kuanza kujitegemea kitaaluma.




