Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewataka wananchi kuwa na subira wakisubiri ripoti ya Tume Maalum iliyoundwa kuchunguza chanzo cha maafa yaliyotokea wakati wa uchaguzi mkuu, huku ikisisitiza kuwa uchunguzi huo unapaswa kuachiwa uhuru bila kuingiliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 23, 2025 jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni, Bw. Garson Msigwa, amesema kuwa ni muhimu kufuata taratibu za Serikali zilizowekwa badala ya kutoa taarifa za upande mmoja.
Bw. Msigwa pia ametoa tahadhari kwa taasisi za habari kutoka nje ya nchi kuepuka kutoa taarifa zisizosahihi na badala yake kufuata maadili ya uandishi wa habari, akibainisha kuwa Serikali iko tayari kutoa ushirikiano pale unapohitajika.
Aidha, amewataka wananchi kujiepusha na kusambaza habari za uchochezi zinazoweza kuligawa taifa, huku akisisitiza kuwa changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni vita ya taarifa, ambayo inalenga kuibua taharuki na kuathiri uchumi wa nchi.

“Watanzania wanataka amani, na kuna baadhi ya watu wanaotumia taarifa potofu kutaka kuvuruga utulivu wa nchi ili kunufaika kisiasa na kiuchumi pindi hali itakapodhoofika,” amesema.
Bw. Msigwa ameongeza kuwa kwa sasa hali ya amani ni shwari, na vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kulinda watu pamoja na mali zao. Hivyo, Watanzania wametakiwa kuendelea kuwa watulivu, kwani Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa nchi zinazotarajiwa kukua zaidi kiuchumi barani Afrika.
Katika hatua nyengine amebainika kuwa Serikali imekemea vikali kitendo kinachodaiwa kufanywa na Shirika la Habari la Kimataifa la CNN, ikikitaja kuwa ni ukiukaji mkubwa na wa makusudi wa misingi ya uandishi wa habari.
Msigwa amesema, hatua za CNN, ambazo amedai zimetofautiana na misingi ya kitaaluma na maadili ya habari, pia zilifanywa na vyombo vingine vya kimataifa vikiwamo BBC, Al-Jazeera na Deutsche Welle.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa, mwenendo huo hauakisi viwango vinavyotakiwa katika utoaji wa taarifa sahihi na zenye uwajibikaji.
“Misingi na maadili ya uandishi wa habari ndiyo nguzo ya kufanya kazi kwa uwazi, usahihi na uwajibikaji. Kitendo hiki ni ukiukwaji mkubwa na wa makusudi,” amesema Msigwa, huku akisisitiza kuwa vyombo vya habari vinapaswa kuzingatia taratibu za kitaaluma ili kulinda hadhi na uaminifu wa taaluma hiyo.


