Serikali kupitia Mradi wa Resilient Natural Resource Management for Tourism and Growth (REGROW) imekamilisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, hatua inayolenga kuimarisha sekta ya utalii, kulinda rasilimali asilia na kukuza uchumi wa Mkoa wa Iringa pamoja na Taifa kwa ujumla.
Leo Februari 10, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, akiambatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa huu, amefanya ziara ya kukagua miradi ya REGROW iliyotekelezwa na kukamilika ndani ya hifadhi hiyo. Miradi hiyo inajumuisha uboreshaji wa miundombinu ya viwanja vya ndege, ujenzi wa malazi ya kisasa pamoja na kuboreshwa kwa huduma zote za msingi zinazowezesha utalii wa kisasa, salama na wenye tija.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Mhe. Kheri amesema kuwa uwekezaji huo umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 59, ukiwa na lengo la kuongeza kwa kiwango kikubwa mvuto wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha katika soko la utalii wa ndani na kimataifa na kusema uwekezaji huo unatarajia kuongeza idadi ya watalii, mapato ya Serikali pamoja na fursa za ajira na biashara kwa wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka hifadhi hiyo.
Aidha, Mhe. Kheri ameongeza kuwa kupitia miradi ya REGROW, Serikali inaendelea kujenga mazingira rafiki ya uwekezaji wa utalii yanayozingatia uhifadhi endelevu wa maliasili sambamba na maendeleo ya kijamii na kiuchumi
Katika hatua nyingine, Mhe. Kheri ametoa wito kwa Watanzania na wageni kutoka mataifa mbalimbali kunufaika na fursa zilizopo ndani ya hifadhi hiyo.
Kwa upande wake, Kamishina Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Bw. Emmanuel Moirana, amesema kuwa hifadhi hiyo ni miongoni mwa wanufaika wakuu wa miradi ya REGROW, ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 95.
Naye Afisa Mhifadhi Mkuu na Msimamizi wa Kitengo cha Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Amina Salum, amesema kuwa miradi hiyo imeleta mapinduzi makubwa katika kuimarisha utalii wa ndani akibainisha kuwa malazi yameboreshwa na idadi ya vitanda imeongezeka, ambapo jumla ya vitanda 158 vimeongezwa pamoja na ujenzi wa hostel yenye uwezo wa kuchukua wageni 126.













