Na WAF, Dodoma

‎Serikali imeendelea kuboresha huduma za watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya wakati (watoto njiti) katika vituo vya afya nchini, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha afya ya mama na mtoto.

‎Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Christina Solomon Mndeme leo Januari 28, 2026 bungeni jijini Dodoma, aliyetaka kujua Je, Serikali ina mkakati gani wa kupanua wigo wa huduma za Watoto Njiti katika vituo vya afya vya mkoa wa Tabora.‎

‎Alisema Serikali imefanikiwa kuongeza vituo vinavyotoa huduma za watoto njiti kutoka hospitali 14 pekee mwaka 2018 hadi kufikia hospitali 362 mwaka 2025 kote nchini.

‎Dkt. Samizi aliongeza kuwa kwa mkoa wa Tabora, huduma hizo zimepanuliwa kutoka vituo sifuri mwaka 2018 hadi kufikia vituo 33 mwaka 2025, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa huduma za watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya wakati pamoja na watoto wachanga wagonjwa.

‎Aliongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa mikakati mbalimbali ikiwemo kusambaza miongozo na vifaa tiba vya kutosha kwenye vituo vya afya, kutoa mafunzo elekezi kwa watoa huduma pamoja na kuongezwa kwa likizo ya uzazi kwa akina mama wanaojifungua watoto njiti.

‎”Serikali itaendelea kuboresha huduma hizo kwa kujenga wodi mpya za kisasa kwa ajili ya watoto njiti, kununua na kusambaza vifaa tiba vya kutosha pamoja na kuendelea kutoa mafunzo kazini kwa watoa huduma ili kuhakikisha watoto wachanga wanapata huduma bora na salama nchi nzima, ikiwemo mkoa wa Tabora.