Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia Dodoma

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezindua rasmi utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mikataba ya Mpango wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji (TACTIC), yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 410 sawa na zaidi ya Shilingi trilioni 1.1, ukihusisha miji 11 nchini.

Uzinduzi huo umefanyika Juni 25, 2026 jijini Dodoma, ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, ameongoza hafla ya utiaji saini mikataba hiyo kati ya Serikali na makandarasi, akisisitiza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni hatua muhimu kuelekea kuboresha maisha ya wananchi wa mijini.

Katika utekelezaji wa awamu hii ya kwanza, Miji ya Morogoro na Songea inajumuishwa kama kundi la awali, huku kundi la pili likihusisha miji ya Tanga, Korogwe, Babati, Shinyanga, Bukoba, Bariadi, Lindi, Iringa na Njombe.

Mchengerwa ameeleza kuwa lengo la mradi wa TACTIC ni kuongeza ufanisi katika usimamizi wa ukuaji wa miji, kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kuziwezesha halmashauri kujitegemea kiuchumi kwa kukuza mapato na mazingira ya uwekezaji.

“Tunahitaji miji ya ushindani ndani na nje ya nchi. Ili kufanikisha hili, halmashauri lazima ziwe na uwezo wa kutoa huduma bora na miundombinu ya kisasa,” alisema Waziri Mchengerwa.

Amebainisha kuwa maeneo ya utekelezaji wa miradi yatakuwa pamoja na ujenzi wa barabara kulingana na vipaumbele vya kila halmashauri, kuboresha masoko ya kisasa, vituo vya mabasi, taa za barabarani na miundombinu ya kisasa ya mawasiliano, ikiwemo wifi na CCTV kwenye maeneo ya masoko na stendi.

Aidha, Mchengerwa ametoa maagizo kwa TARURA kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi hiyo na kutengua mikataba ya makandarasi wote watakaoshindwa kukamilisha kazi kwa wakati au watakaohamisha fedha kwenda miradi mingine kinyume na taratibu.

“Wapo baadhi ya makandarasi ambao wakishalipwa wanaenda kutekeleza miradi mingine badala ya hii waliyopewa. Hatuwezi kuvumilia hali hii. Tengueni mikataba yao mara moja,” alisisitiza.

Amesisitiza pia ushirikishwaji wa wananchi wa maeneo husika kwa kuwapa ajira ndogo ndogo kwenye miradi hiyo, huku akitoa wito kwa wakurugenzi wa halmashauri kutoa usaidizi kwa wakandarasi kwa lengo la kuhakikisha miradi inakamilika mapema na kwa ubora.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, Rogatus Mativila, amesema jumla ya miji 45 inatarajiwa kunufaika na mradi huu kwa kipindi chote cha utekelezaji, na kwamba miji 11 iliyoanza ni sehemu ya awamu ya kwanza.

“Mradi huu unahusisha majiji 5, manispaa 16 na miji 24 kote nchini. Lengo ni kuiandaa Tanzania kuwa na miji yenye mvuto wa kiuchumi, huduma bora na mazingira rafiki kwa wawekezaji,” amesema Mativila.

Katika hafla hiyo, baadhi ya wabunge walioshiriki wakiwemo Hamida Mohammed (Lindi Mjini) na Ummy Mwalimu (Tanga Mjini) walimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuwekeza kwenye miundombinu ya miji ambayo ilikuwa imebeba changamoto kubwa kwa miongo mingi.

Mbunge wa Lindi, Hamida Mohammed, ameeleza kuwa mradi wa ujenzi wa Soko Kuu la Lindi ni mkombozi mkubwa kwa wananchi ambao kwa zaidi ya miaka 50 wamekuwa wakitumia soko chakavu lisilo na miundombinu ya msingi, hususan wakati wa mvua.

“Soko letu jipya litakuwa na vizimba vya kisasa, maduka, mabucha, maeneo ya kuuza samaki wakavu, kituo cha mabasi ya soko, mfumo wa usalama na huduma za kisasa kama Wi-Fi na CCTV,” alieleza kwa furaha.

Amesema kwa ujumla Serikali kupitia TACTIC imeonesha dhamira ya kweli ya kuleta mabadiliko ya kimkakati katika ustawi wa miji kwa kuwekeza katika miundombinu itakayosaidia si tu huduma bora, bali pia kukuza uchumi wa maeneo na taifa kwa ujumla.