Na Mwandishi Wetu

Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) yametakiwa kuwa wazi na kuwajibika katika utekelezaji wa majukumu yao, hasa katika kutoa huduma kwa wananchi kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Wito huo ulitolewa juzi na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, wakati akifungua Kongamano la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa mwaka 2025, linalofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, kuanzia Agosti 11 hadi 13.

Mwanaidi alisema uwazi na uwajibikaji ni msingi muhimu wa kutambua mchango wa NGOs katika maendeleo ya Taifa, na kusisitiza umuhimu wa mashirika hayo kushirikiana kwa karibu na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo.

“Viongozi na wasimamizi wa miradi ya kimaendeleo katika mashirika yenu, nawaomba kuzingatia uwajibikaji pamoja na kuwa tayari kubadilishana uzoefu ili kufanikisha maendeleo endelevu ya Taifa letu,” alisema Mwanaidi

Aidha aliwahimiza kutoa elimu ya kiraia kwa wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao, ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kidemokrasia kwa kuzingatia haki na wajibu wao.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Wakili Amon Mpanju, amesema kuwa NGOs ni nyenzo muhimu katika utoaji wa huduma kwa jamii, na kuyataka mashirika hayo kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha wananchi wananufaika ipasavyo na miradi inayotekelezwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Bi. Mwantum Mahiza, amesema kuwa Bodi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha mashirika yanazingatia kanuni, taratibu na maadili ya kazi ili kufanikisha maono yao kwa jamii.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Bw. Gasper Makala, alieleza kuwa Baraza hilo limeweka mikakati madhubuti ya kuimarisha ushirikiano kati ya NGOs, Serikali na wadau wengine kwa lengo la kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Kongamano hilo la mwaka linafanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Tathmini ya Miaka Mitano kuhusu Mchango wa NGOs katika Maendeleo ya Taifa 2020/2021–2024/2025: Mafanikio, Changamoto, Fursa na Matarajio.”