Takriban watu 22 wameuawa na wengine 63 kujeruhiwa katika shambulio la bomu la kujitoa muhanga katika kanisa moja mjini Damascus, wizara ya afya ya Syria imesema.
Mwanamume mmoja alifyatua risasi kwa kutumia silaha katika Kanisa la Kiorthodoksi la Ugiriki la Nabii Elias katika kitongoji cha Dweila wakati wa ibada ya Jumapili jioni kabla ya kulipua vilipuzi, kulingana na wizara ya mambo ya ndani.
Ilisema mshambuliaji huyo alikuwa na uhusiano na kundi la wanajihadi la Islamic State (IS). Hakukuwa na madai ya mara moja kutoka kwa kundi lenyewe.
Picha na video kutoka ndani ya kanisa zilionyesha madhabahu iliyoharibiwa sana, viti vilivyofunikwa kwa vioo vilivyovunjika na damu iliyotapakaa kwenye kuta.
