*Awataka vijana kutulia, ataka vyombo vya habari kuwa makini
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kagera
Watanzania wameombwa kuendelea kutunza na kulinda amani, umoja na mshikamano kwa nguvu zote kwa sababu ndio msingi mkubwa wa kupata maendeleo na mahitaji mengine.
Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Sheikh wa Mkoa wa Kagera, Haruna Kichwabuta, wakati akizungumza na JAMHURI juu ya umuhimu wa Watanzania kuendelea kulinda amani, baada ya vurugu za Oktoba 29, mwaka jana zilizosababisha uharibifu mkubwa wa mali na kusababisha vifo vya watu kadhaa.
“Bila ya kuwepo amani, hakuna kitu kinaweza kufanyika isipokuwa ni madhara, tumeona namna hali ilivyokuwa kipindi cha nyuma, kila mmoja ni shuhuda wa matukio ya Oktoba 29, mwaka jana, hatuna sababu ya kurudi huko, mahubiri ya viongozi wa dini na viongozi wa siasa yasiwe ya ubinafsi.
“Kama hakuna amani, hakuna kwenda hata msikitini siku ya Ijumaa au kwenda kanisani siku ya Jumapili, wala kusoma ibada za usiku kama ambavyo tumezoea.
“Kama hakuna amani hamuwezi kufanya mikusanyiko, utamhubiria nani? Kazi za viongozi wa dini siku zote ni kuhubiri amani pamoja na kuiombea nchi.
“Mara nyingi viongozi wa dini wamekuwa wakitengeneza mikutano mikubwa kuomba maombi na kuwaombea watu, wasiache kuwasisitiza suala la Amani, kwa sababu hata leo hii tunazungumza kwa sababu ya uwepo wa amani.
“Hakuna sheikh wala padri kama amani ikikosekana. Hivi vyeo vyote tunavyo kwa sababau amani ipo na ukikumbuka kuwa hakuna aliyekuja na cheo na hata sasa ukiangalia hizi nchi tunazoziona zinaendelea kurushiana maneno utagundua kuwa hakuna amani,” amesema.

Amesema sehemu yoyote ambayo haina amani itakuwa vigumu watu kwenda kusali maana misikiti na makanisa na hata majengo ya hospitali hubomewa.
“Katika kazi wanazotakiwa kufanya viongozi wa dini kwa moyo ni kujitoa kwenye mambo ya siasa na kuhubiri amani kwa waumini wetu ili waweze kutuisikia.
Kuhusu vijana, Sheikh Kichwabuta amesema wanapaswa kutambua ujana wao unapata heshima kwa sababu amani ipo na kama haitakuwapo, basi hakuna heshima kwao, maana watakuwa wahuni, wezi na mwisho wa siku watapoteza maisha.
“Ili ujana upate heshima, vijana wanatakiwa kutulia, kama wamesoma na hata ambao hawakufikia hatua ya kusoma pia watulie.
“Tutaona vijana wako barabarani wakishinikiza kupata kazi bila kujua kuwa hauwezi kushinikiza upate kazi wewe mwenyewe, bali utaleta matatizo, maana tangu zamani kuna utaratibu wa kupata kazi, watu wengine huishi kwa mbinu mbalimbali, si kupata mishahara ya serikali, watu wasiwe na fikra hizo,” amesema.
Amesema viongozi wa dini wanatakiwa kutoa somo na darasa kwa vijana kuangalia nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Sudan ambazo zimekuwa na machafuko, wakati nchi kama Burundi wananchi wake wengi wamekuwa wakimbizi ndani ya Tanzania.
“Leo tunarudisha watu Burundi, hawa hawajakimbia nchi yao kwa kupenda, ni kwa sababu ya kuvurugika amani, ninawasihi vijana wajifunze kuheshimu serikali.
“Siku zote lazima tuwe na utawala, ukiangalia sisi miaka 60 sasa, tunajua hakuna atakayedumu, maana hatutaletewa Mungu wala malaika, sasa ukisema uwatoe kwa nguvu haitawezekana.
“Viongozi wa dini na siasa waache ubinafsi. Mimi ningekuwa hivi, inakuwa vile au ningefanya vile, ukiangalia hata Mwalimu Julius Nyerere alipata taabu tangu tukiwa watu milioni nane na sasa tuko milioni 60, tuache kujiona sisi ni bora kuliko wengine, bali tufuate utaratibu tutafika.,” amesema.
Kuhusu mitandao ya kijamii, Sheikh Kichwabuta amesema imechangia kuwapo matatizo makubwa katika jamii.
“Mitandao hii ina faida zake, lakini katika siku za karibuni imeonekana kuchangia matatizo kwa vijana wetu, vitu wanavyoviona vinakuja kuleta matatizo huku, maana wanafanya majaribio ya vile wanavyoiviona mitandaoni,” amesema.
Katika hatua nyingine, amewaasa waandishi wa habari kutumia kalamu zao vizuri kwa sababu kinyume cha hapo wanaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
“Nawasihi watu wa habari, wanatakiwa kutumia vizuri kalamu zao ili kudumisha Amani, si kuhamasisha chuki,” amesema.

