Na OWM – TAMISEMI, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amewataka Waheshimiwa Madiwani nchini kuwa wanyenyekevu kwa wananchi katika kuwatumikia na kuwaletea maendeleo.
Prof. Shemdoe ametoa wito huo kwa Madiwani hao leo, wakati akimuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba katika kikao kazi na madiwani hao kilichofanyika katika Ukumbi wa CCM Makao Makuu jijini Dodoma.
“Sisi viongozi hatutakiwi kuwa na kiburi tunatakiwa kuwa wanyenyekevu kwa wananchi waliotuchagua, Petro wa kwanza sura ya tano mstari wa tano inasema Mungu huwapinga wenye viburi lakini huwapa wanyeyekevu neema, kwa hiyo sisi viongozi hatupaswi kuwa na kiburi”, amesisitiza Prof. Shemdoe.
Aidha, Prof. Shemdoe amewapongeza Waheshimiwa Madiwani hao kwa Azimio lao la kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utendaji kazi wake ulioleta mageuzi makubwa katika sekta ya uchumi, kilimo, mifugo na uvuvi, ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi hususani walio pembezoni.
Akizungumza kwa niaba ya Madiwani, Katibu wa Madiwani Bi. Hilda Kadunda amesema wanafarijika kuona namna Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyoendelea kupambana kukuza uchumi, kuongeza wigo wa ajira kwa vijana, kuvutia ushiriki wa vijana katika kilimo, mifugo na uvuvi, kutekeleza sera ya Bima ya Afya kwa wote, ujenzi wa bwawa la umeme na reli ya kisasa (SGR).
Kwa upande wake, Katibu Mwandamizi wa CCM Makao Makuu Bw. Adam Ngalawa amesema Wabunge na Madiwani wana dhamana kubwa ya kuongoza watu, na kuongeza kuwa, wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa niaba ya Mhe. Rais hivyo kila wanachofanya kinapaswa kuendana na haiba ya Mhe. Rais, kinyume na hapo ni kumuangusha Mhe. Rais, Chama kilichowaweka madarakani na wananchi walio wachagua.




