Shirika la ndege la gharama nafuu kutoka Ireland, Ryanair, limeibuka na mpango mpya unaolenga kubadili kabisa taswira ya usafiri wa anga – kwa kuondoa viti kwenye baadhi ya safari zake na kuanzisha mfumo wa abiria kusimama.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa vyanzo vya ndani ya kampuni hiyo, Ryanair iko katika hatua za majaribio ya teknolojia maalum ya mikanda ya usalama inayowekwa ukutani, itakayowawezesha abiria kusimama kwa muda wote wa safari huku wakiwa wamefungwa kwa usalama.
Mpango huu unalenga kuanzishwa kwenye baadhi ya safari maalum, ikiwa ni pamoja na zile za umbali mrefu. Mfano uliotajwa ni safari ya kutoka Tanzania hadi Ufaransa, safari ya takribani masaa 9 angani, ambapo nauli yake inasemekana kuwa ni euro 10 tu — sawa na takriban shilingi 30,000 za Kitanzania.
Lengo? Kuwahudumia Wasafiri wa Kipato cha Chini
Kwa Ryanair, lengo ni kuwafikia watu wengi zaidi, hususan wale wa kipato cha chini wanaotamani kusafiri nje ya nchi kwa gharama nafuu — bei inayolingana na usafiri wa treni au basi ndani ya nchi.
Je, Ni Salama?
Ingawa teknolojia hiyo ipo kwenye hatua za majaribio, wasiwasi kuhusu usalama wa abiria katika safari za muda mrefu huku wakiwa wamesimama bado unaendelea kujadiliwa vikali kwenye sekta ya usafiri wa anga na kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii.
Swali la Msingi:
Je, uko tayari kusimama kwa masaa 9 angani kwa bei sawa na soda na maandazi?
Ni ubunifu au ni kero mpya kwa abiria?
