Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
SHIRIKA la Posta Tanzania ni miongoni mwa washiriki katika kongamano la 18 la eLearning Afrika ambapo limetambulisha huduma ya ‘Swifpack’.
Swifpack inalenga kuchukua vifurushi na abiria kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa urahisi kupitia simu janja.
Akizungumza na waandishi wa habari, leo Mei 09, 2025 katika banda lao lililopo katika kongamano hilo, Kaimu Meneja Mauzo Shirika la Posta Tanzania, Andrea Liundi amesema Swifpack inalenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kurahisisha usafirishaji wa mizigo au vifurushi.
“Kupitia maonesho haya ya eLearning Afrika, Shirika la Posta liko hapa kwaajili ya kutoa huduma kwa washiriki hasa wageni ambao wametoka nje kwaajili ya kushiriki hili kongamano.
“Pamoja na mambo mengine tuliyonayo, pia tumekuja na huduma ya Swifpack ambayo unadownload application kupitia simu janja. Kwamaana sasa hivi sio lazima uje ofisini kwetu kama unahitaji kutuma kifurushi bali unaingia Swifpack halafu unaita pikipiki au bajaji au gari,” amesema.
Ameongeza kuwa, katika kongamano hilo pia wanatoa huduma ya kusafirisha vifurushi kwenda ndani ya Tanzania na nje ya nchi.
“Lakini kikubwa zaidi hapa tupo kwaajili ya kutoa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni. Tumeona kwamba wageni wakija hapa wanahitaji kubadilisha fedha na kupata za kitanzania kwaajili ya kufanya manunuzi yao ya ndani.
“Na tunashukuru muitikio ni mzuri tangu tumeanza juzi tumeweza kupata wageni wengi ambao wameenda kubadilisha fedha, pia Watanzania wameenda wanahitaji Dola. Na hiyo imetufanya tunatoa huduma hata nje ya muda wa kazi na hii ndo inaonesha jinsi gani kunauhitaji wa hii huduma,” amesema.
