Na OWM – TAMISEMI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe ameridhishwa na maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wa darasa la awali na la kwanza katika Shule ya Msingi Iyumbu jijini Dodoma, na kuuarifu umma kuwa maandalizi katika shule zote za msingi 18055 yamekamilika na zipo tayari kupokea wanafunzi kuanzia Januari 13, 2026.

Prof. Shemdoe amesema, ameitembelea shule hiyo ya Msingi Iyumbu leo Januari 12, 2026, ili kujiridhisha na maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wanaotarajiwa kuanza darasa la awali na la kwanza Januari 13, 2026 na amejionea mwenyewe kuwa maandalizi yamekamilika.

“Tumeona maandalizi kwenye shule hii yamekamilika, kama ilivyo kwenye shule zote 18055 za msingi, hivyo natoa wito kwa wazazi wenye watoto walio na umri wa kuanza darasa la awali na la kwanza wawapeleke shuleni,” Prof. Shemdoe amesisitiza.

Prof. Shemdoe amejionea madarasa ya awali mazuri ambayo yamejengwa kwa fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, na kuzielekeza halmashauri zote nchini kutumia mapato ya ndani kujenga miundombinu bora ya elimu kama ambavyo Halmashauri ya Jiji la Dodoma imejenga katika Shule ya Msingi Iyumbu.

Aidha, Prof. Shemdoe amewataka walimu nchini kuhakikisha shule zinatoa wanafunzi wenye ufaulu mzuri kwani Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu, hivyo ufaulu wa wanafunzi ni faraja kwa Mheshimiwa Rais.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema kwamba tangu Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani ufaulu umeongezeka, na kuongeza kuwa sababu kubwa ya kuongezeka kwa ufaulu huo ni uwekezaji fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya elimu.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Iyumbu, Bi. Monica Nshimba amemshukuru Prof. Shemdoe kwa kuitembelea shule yake na kumuahidi kwamba walimu wako tayari kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kutimiza lengo la Serikali la kutoa elimu bora ya msingi kwa wananchi wake.

Naye, Diwani wa Kata ya Iyumbu Mhe. Sadiki Mponyamili amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia kata yake fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha Shule ya Msingi Iyumbu na ameipatia kata yake zaidi ya Shilingi Milioni 150 kwa ajili ya kuboresha shule ya Sekondari.