Na Manyerere Jackton, JamhuriMedia

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ni chombo nyeti. JWTZ ndiyo taasisi iliyoendelea kukosha nyoyo za Watanzania tangu kuanzishwa kwake miongo mingi iliyopita.

Unyeti wake unatulazimu sote tunapoijadili, tuijadili kwa weledi, staha na kutambua dhima kubwa iliyonayo kwa usalama na uimara wa taifa letu.

Mambo yanayoendelea bungeni yakiachwa yastawi yatavuruga misigi ya utendaji kazi wa Jeshi letu.  Watumishi wa JWTZ hawawezi kujadiliwa kama waombaji wengine wa ajira za ujenzi wa barabara, majengo, na kadhalika; na ndiyo maana askari wa JWTZ hawaajiriwi, bali wanaandikishwa, kwani hakuna mtu anaajiriwa kwenda kufa, bali anaandikishwa [anajitolea] kwenda kufa kwa ajili ya ulinzi wa taifa lake.

JWTZ inalazimika kisheria na kitaaluma kuwachukua vijana mahiri na makini-wenye nidhamu na weledi wa kuliotumikia taifa. Siyo kuchukua vijana tu kwa kigezo cha kugawana au kupeana ajira. Maovu mengi tunayoyaona ndani ya baadhi ya vyombo vya usalama yanatokana na kupeana ajira kienyeji. Hili lisipenyezwe JWTZ.

Wabunge wasiamini kuwa  kazi zinazotangazwa ndani ya JWTZ ni jawabu la uhaba wa ajira nchini. Jeshi hili halipo kwa ajili ya kupunguza uhaba wa ajira, bali kwa ajili ya kulinda mipaka na uhuru wa Tanzania.

JWTZ iliundwa kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ya mwaka 1966, inayojulikana kama The National Defence Act, 1966 (Cap. 192). Sheria hii iliianzisha JWTZ kuwa jeshi la kudumu la ulinzi kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikifuta rasmi jeshi la awali la Tanganyika Rifles lililorithiwa kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza. Sheria hii iliweka msingi wa muundo wake, dhima yake ya msingi (kulinda uhuru, mipaka, na mamlaka ya nchi), taratibu za ajira, nidhamu na utawala wa wanajeshi, na ushirikiano wa JWTZ na mamlaka ya kiraia.

Kikatiba na kisheria, Bunge lina mamlaka ya kutunga sheria zinazohusu uajiri na uendeshaji wa majeshi, ikiwamo JWTZ. Hata hivyo, Bunge halipaswi kuingilia moja kwa moja taratibu za kila siku za ajira au utendaji wa majeshi kwa sababu hiyo ni kazi ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, ambaye sasa ni Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa muktadha huu, Bunge kazi zake hapa ni kutunga sheria za kuanzisha au kurekebisha taratibu za jumla za uajiri na utumishi wa wanajeshi (kupitia The National Defence Act).

Kuidhinisha bajeti ya Jeshi ambayo inabeba idadi ya askari, vifaa, mishahara, nk. Kuwajibisha Serikali kuhusu sera za ulinzi na matumizi ya nguvu za kijeshi kupitia kamati maalumu za Bunge; kuchunguza malalamiko ya ukiukwaji wa haki au matumizi mabaya ya mamlaka katika ajira za kijeshi kwa njia ya kiutawala, si kiutendaji. Hapa muhimu ni kuzingatia hayo maneno mawili-kiutawala na kiutendaji.

Kwa upande wa pili, Bunge halina mamlaka ya kuamuru ajira ya mtu fulani katika jeshi, kuingilia mchakato wa kupandisha au kushusha vyeo, kutoa maagizo ya moja kwa moja kuhusu uteuzi, mafunzo au uhamisho wa wanajeshi, kuvunja misingi ya siri, ufanisi na weledi wa kijeshi kwa siasa au ushawishi wa nje.

Bunge lina mamlaka ya kisera na kisheria juu ya majeshi, lakini si ya kiutendaji. Ulinzi wa taifa unahitaji mfumo wa kijeshi usiotawaliwa na siasa za kila siku, bali unaoongozwa na utaalamu, nidhamu, na amri za kijeshi. Hii ndiyo sababu jeshi linabaki kuwa taasisi ya kipekee inayofanya kazi chini ya Serikali, lakini kwa kuzingatia sheria zilizotungwa na Bunge. Nje ya Amiri Jeshi Mkuu, hakuna mtu au chombo chenye mamlaka ya kuliamuru Jeshi kufanya hiki, au kutofanya kile. Mamlaka nyigine zote-Bunge, Waziri wa Ulinzi, CDF, au Baraza la Mawaziri-zinashiriki kiutawala, kisera, au kwa ushauri

Na si kutoa amri zinazotakiwa kutekelezwa kijeshi kama hii ya aina ya vijana wanaochukuliwa kujiunga.

Baada ya JWTZ kuundwa rasmi, Bunge lilitunga sheria mpya ya ulinzi, ambayo haiingilii utendaji wa ndani wa JWTZ. Serikali iliweka msimamo kwamba jeshi halitakuwa la kisiasa na halitawajibika moja kwa moja kwa Bunge, bali kwa Serikali (kupitia Rais na Waziri wa Ulinzi).

Hii ina maana kwamba Bunge linapaswa kutunga sheria nzuri na kuweka mifumo ya usimamizi wa kisera, lakini lisiiingilie moja kwa moja uajiri au utendaji wa kijeshi, kwani hilo linaweza kusababisha migogoro au kuyumbisha ulinzi wa taifa.

Kwa nini Jeshi lina haki ya kuajiri vijana waliopitia JKT?

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwapo mijadala kuhusu uhalali wa JWTZ kuajiri vijana waliopitia JKT pekee. Wapo wanaodhani kuwa hatua hii ni ubaguzi, lakini kwa uchambuzi wa kina, ni wazi kuwa uamuzi huu una msingi wa kitaaluma, kiutendaji, na hata wa kisheria.

JKT ni kiwanda cha maandalizi ya kijeshi. JKT si kambi ya kawaida, bali ni taasisi ya serikali iliyoanzishwa kwa lengo la kuwaandaa vijana katika misingi ya uzalendo, nidhamu, kazi, mshikamano wa kitaifa na ulinzi wa taifa. Hii inamaanisha kuwa JKT ni daraja rasmi la maandalizi ya maisha ya kijeshi. Ni sawa na chuo cha mafunzo ya awali kwa taaluma yoyote — kama vile Chuo cha Polisi kwa askari wa polisi au vyuo vya ualimu kwa walimu.

Hivyo basi, kwa mtazamo wangu, JWTZ kuajiri waliopitia JKT si ubaguzi, bali ni uteuzi wa wale waliokwisha andaliwa na mfumo rasmi kwenda kufanya kazi hii ngumu na muhimu kwa ulinzi wa taifa letu.

Vijana waliopitia JKT hujengwa kiakili, kimwili na kimaadili. Wanajifunza nidhamu, kuheshimu mamlaka, kufanya kazi kwa ushirikiano, kuvumilia mazingira magumu na kuweka mbele maslahi ya taifa. Sifa hizi ndizo zinazotakiwa kwa mwanajeshi wa JWTZ. Kuajiri vijana waliokwishazipata kupitia JKT ni njia ya kuhakikisha Jeshi linabaki na watumishi wenye maadili, moyo wa kizalendo na utayari wa kulinda nchi.

Jeshi ni taasisi nyeti inayogusa moja kwa moja usalama na mamlaka ya taifa. Si kila kijana mwenye afya au elimu anaweza kuingia JWTZ. Ni lazima apimwe kwa vigezo vya kipekee. JKT huandaa vijana kwa misingi hii. Kuwaingiza watu wasiopitia mfumo huu ni kuhatarisha ufanisi na mshikamano ndani ya jeshi; jambo linaloweza kuwa na athari kubwa kwa usalama wa taifa.

Ni muhimu pia kufahamu kuwa JKT ni wazi kwa vijana wote wa Kitanzania. Ingawa idadi ya wanaopokewa inaweza kuwa ndogo kutokana na rasilimali zilizopo, hakuna ushahidi kuwa kuna makundi yanabaguliwa kimakusudi.

Serikali inaweza kuimarisha mfumo huu kwa kuongeza bajeti na miundombinu ili vijana wengi zaidi wapitie JKT na kuongeza nafasi ya kuingia JWTZ. Hii ni kazi ya wabunge kuhakikisha wanaibana Serikali ili vijana wengi wajiunge JKT.

Mwandishi wa makala hii, Manyerere Jackton akiwa na baadhi ya makamanda wa JWTZ kwenye Operesheni Demokrasia, Kisiwani Anjouan nchini Comoro.

Wabunge wajue kuwa Jeshi si taasisi ya ajira ya umma ya kawaida kama zilivyo taasisi nyingine. Hii si ajira ya viwandani au ujenzi wa barabara!

Tofauti na taasisi nyingine za umma, Jeshi lina mahitaji maalum ya kitabia na kimwili. Si sehemu ya kujaribu “kusaidia vijana wote”, bali ya kuwachagua wale walio tayari kufa kwa ajili ya taifa. Hili linahitaji mafunzo na uchunguzi wa kina kabla ya mtu kuaminiwa kuvaa sare ya JWTZ. Hii ndiyo maana JKT ni nguzo muhimu ya uchujaji.

Kuna haja kwa wabunge hawa kuelewa kuwa kuajiri vijana waliopitia JKT si ubaguzi, bali ni uteuzi wa kitaalamu unaoendana na mahitaji ya kiutendaji ya Jeshi.

Badala ya kulalamikia utaratibu huu, juhudi zielekezwe katika kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata nafasi ya kwenda JKT ili kuongeza usawa wa fursa. Ni kwa njia hii ndipo taifa litakuwa na Jeshi imara, lenye nidhamu, na linalotokana na maandalizi rasmi ya kizalendo.

Katika mjadala uliopo bungeni kuhusu ajira JWTZ, kunasikika sauti za wabunge wanaopendekeza kwamba kipimo cha kupitia JKT kisiwe tena kigezo cha kujiunga na JWTZ. Hoja hii, ingawa inaonekana kuheshimu kanuni za usawa wa fursa, ina upungufu mkubwa wa kitaaluma, kikatiba na kiusalama. Upungufu huo unaweza kuathiri utendaji na mshikamano wa jeshi letu.

Wabunge wanaodai kwamba JKT ni kizuizi cha usawa watambue kuwa JKT bni taasisi rasmi ya mafunzo ya msingi ya kijeshi na uzalendo. Ilianzishwa kwa msingi wa Kifungu cha 124 cha Katiba ya Tanzania (1977) na sheria ya JKT (Sura 179), kusudi lake ni kuandaa vijana kiakili, kimwili na kimaadili kwa huduma ya taifa. Kuondoa thamani ya mafunzo haya ni sawa na kupunguza umuhimu wa chuo chochote cha mafunzo ya kitaaluma.

Kikatiba, JWTZ ina mamlaka ya kuweka vigezo vya kujiunga vinavyolenga kuhakikisha uadilifu, nidhamu na ufanisi wa kijeshi (Katiba ya Tanzania, Kifungu cha 131[1]).

Mahitaji ya JKT yameundwa kwa kuzingatia misingi ya usalama na ulinzi, yaliidhinishwa Bungeni na Kamati ya Ulinzi. Wabunge wanapopendekeza kuondoa kipimo hiki, wanavunja mchakato wa kikatiba wa kuweka sera za ajira za jeshi.

Jeshi la taifa lolote makini linategemea nidhamu, mshikamano na uwezo wa kukabiliana na hatari. JKT huchuja na kuandaa vijana walio na sifa hizi; ni hatua ya awali ya uchunguzi wa kisaikolojia, kiafya na kiitikadi. Kupunguza au kuondoa kipimo cha JKT kutasababisha kuajiri watu wasiopitia uchunguzi huu wa kina; jambo linaloweza kupunguza uwezo wa operesheni za JWTZ na kuongeza hatari kwa usalama wa nchi.

Wabunge wanaogopa ubaguzi wanasisitiza usawa wa fursa (“equality of opportunity”) bila kuelewa kuwa katika sekta nyeti kama ulinzi, muhimu zaidi ni “usawa wa matokeo” (“equality of outcome”)—yaani kuhakikisha kila mwanajeshi ana sifa na maandalizi sawia. JKT ni chombo kinachosababisha usawa wa matokeo kwa kuwapa vijana kutoka sehemu zote za nchi mafunzo sawia. Badala ya kuondoa kipimo, kama nilivyoanza kusema awali, ni vyema kuboresha upatikanaji wa JKT kwa kuwafikia vijana wote- wakiwamo wa familia maskini na walioko pembezoni.

Ningekuwa mbunge, badala ya kushupaa kuondoa vigezo vya JKT, ingependekeza kuongeza bajeti na miundombinu ya JKT. Ningependekeza upanuzi wa uwezo wa kambi na mafunzo ili kuhudumia idadi kubwa ya vijana.

Nionavyo mimi, kujenga Jeshi imara na linaloeleweka, kuondoa kipimo cha JKT ni suluhisho la haraka lisilo na msingi imara wa kudumu. Wabunge waliotoa pendekezo hili wanapaswa kuelewa kwamba sera za ajira za jeshi lazima ziakisi mahitaji ya usalama wa taifa, na si mitazamo ya kisiasa ya muda mfupi.

Ni jukumu la wabunge kutetea na kuboresha mfumo wa JKT, ili kila kijana mwenye uwezo awe na fursa ya kupitia mafunzo haya muhimu. Hii ndiyo njia ya kuhakikisha JWTZ inabaki na nguvu, nidhamu na ufanisi unaotokana na maandalizi rasmi na ya kitaaluma.

Kwa hiyo, Bunge hutoa muundo wa kisheria na rasilimali, kisha Jeshi kupitia Wizara ya Ulinzi na Amiri Jeshi Mkuu hufafanua na kutekeleza sifa na aina ya watu wanaoajiriwa.

Siamini kuwa uwezo wa wabunge wetu kuona nchi inaandaa ajira umekomea kwenye nafasi kama hizi za Jeshi. Vijana wa Tanzania wenye umri wa miaka 18-35 [kwa sensa ya mwaka 2022] ni karibu asilimia 35 ya Watanzania wote, yaani vijana karibu milioni 24.

Idadi hii ya vijana itapata ajira endapo Bunge na serikali waakuja na sheria na sera madhubuti za kuwapatia kazi za uzalishaji, na si kuhangaika na ajira za JWTZ ambazo kwa wakati mmoja hata hazifiki 5,000. Tukumbuke kuwa Jeshi si juu ya ajira, bali ni suala la ulinzi wa taifa.

0759 488955