📌Serikali yatoa zaidi ya Shilingi Bil 500 kulipa makandarasi‎

‎Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeweka historia mpya katika eneo la King’ori, jijini Arusha na maeneo mengine nchini kwa kuweka tumaini jipya kwa wananchi kupitia ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja ndani ya siku 100 za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.‎

‎Hayo yameelezwa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega wakati akizungumza na waandishi wa Habari pamoja na wananchi wa King’ori jijini Arusha kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Ujenzi ndani ya Siku 100 za Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani.‎

‎Ulega ameeleza kuwa pia Serikali kupitia Wakala huo imekamilisha ujenzi wa miradi 40 ya madaraja ya dharura kati ya 81 ikiwemo hapo Kingo’ri yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 500 ambayo inatekelezwa chini ya programu maalumu ya Contingent Emergency Response Component (CERC), ambapo ameeleza kuwa miradi yote imekwenda kutatua changamoto na kuleta tabasamu kwa wananchi.‎

‎Ulega ameongeza kuwa Serikali imetoa fedha hizo ndani ya siku 100 kwa ajili ya kulipa makandarasi waliotekeleza miradi ya ujenzi nchini na kusisitiza kuwa kati ya fedha hizo shilingi Bilioni 280 zimetoka Hazina na nyingine zilizobaki zimetoka kwa wafadhili.‎

‎Waziri Ulega amesema kuwa mbali na ujenzi wa madaraja Sita makubwa ya kupitisha maji kutoka milimani katika eneo la King’ori, pia Serikali imefanikiwa kuweka jumla ya taa 136 za barabarani, ujenzi wa kilometa moja ya lami pamoja na Ujenzi wa vituo viwili vya daladala ambapo amesema kuwa Serikali imefanikisha huduma hizo ili kuleta tabasamu la utu kwa wananchi wa eneo hilo.‎

‎“Moja ya mafanikio yaliyopatikana katika siku 100 ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya hapa King’ori, wenyeji wenyewe wanayo simulizi kubwa kwani mahala hapa hapakuwa na madaraja makubwa ya kupitisha maji, lakini ndani ya siku hizi tulihakikisha tunajenga na kukamilisha mradi huu”, amesema Ulega.‎

‎Ulega ameongeza kuwa katika siku 100 za Dkt.Samia, Wizara yake pia imeanza kutatua changamoto ya foleni katika eneo la Rangi Tatu (Mbagala) hadi Kongowe jijini Dar es Salaam katika maingilio ya barabara ya Mkuranga kuelekea Kusini ambapo amesema kuwa Rais Samia alitoa shilingi Bilioni 16 za fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi huo na kutoa fedha za awali za ujenzi takribani shilingi Bilioni Tisa.‎

‎Kwa upande wake, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Mhe. Joshua Nassari ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo inagusa wananchi moja kwa moja ikiwemo ujenzi wa madaraja, vituo vya mabasi na taa katika jimbo lake.