Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Wizara ya Nishati kwa kazi kubwa inayoendelea kutekelezwa ndani ya siku 100 za uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo kuanza kusambaza umeme katika vitongoji 9,009, hatua inayoonesha mwelekeo chanya wa utendaji wa kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Sita.

Pongezi hizo zimetolewa Januari 20, 2026 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Subira Mgalu, wakati wa kikao cha kwanza kati ya Wizara ya Nishati, taasisi zilizo chini yake pamoja na Kamati hiyo.

Kikao hicho kimelenga kuijengea Kamati uelewa kuhusu muundo na majukumu ya Wizara ya Nishati, pamoja na sera na sheria mbalimbali zinazosimamiwa na Wizara hiyo katika kuendeleza Sekta ya Nishati nchini.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mgalu amesema mafanikio yaliyopatikana ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Samia ni ushahidi wa dhamira ya Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa wananchi.

“Niwapongeze sana Wizara ya Nishati na taasisi zake kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya katika kuijenga Sekta ya Nishati. Mafanikio haya yamejidhihirisha wazi ndani ya siku 100 za uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tumeshuhudia uzinduzi wa Kituo cha Umeme cha Mtera ambacho kitaimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Dodoma na Iringa, pamoja na uzinduzi wa mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 9,009 nchini,” amesema Mgalu.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema Wizara itaendelea kuhakikisha Sekta ya Nishati inachangia ipasavyo katika kufikiwa kwa malengo ya kitaifa na kimataifa, sambamba na kukuza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya Taifa na ustawi wa wananchi.

Amebainisha Serikali itaendeleza matumizi ya vyanzo mbalimbali vya nishati ambavyo Tanzania imebarikiwa navyo ili kufanikisha mpango wa kuzalisha megawati 8,000 za umeme ifikapo mwaka 2030, pamoja na kuongeza matumizi ya umeme kwa wananchi hadi kufikia wastani wa kilowati saa (KWh) 3,000 kwa kila mtu ifikapo mwaka 2050.

Kuhusu nishati safi ya kupikia, Mhe. Ndejembi amesema Wizara inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, kuongeza vituo vya upatikanaji wa nishati hiyo pamoja na kubuni na kuendeleza teknolojia rafiki kwa mazingira.

Aidha, ameahidi kuwa Wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu na Kamati hiyo na kuzingatia maoni na ushauri wa Kamati hiyo katika utekelezaji wa majukumu yake kwa maendeleo ya Sekta ya Nishati na Taifa kwa ujumla.

Viongozi wengine wa Wizara ya Nishati waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.