Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi George Simbachawene, ameipongeza Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa kubuni na kuzindua mfumo wa short code unaolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za vitambulisho vya taifa kwa wananchi kupitia simu za mkononi.
Akizungumzawakati wa uzinduzi wa mfumo huo uliofanyika katika ofisi za NIDA, Simbachawene amesema huduma hiyo ya ujumbe mfupi wa simu (SMS) itawawezesha wananchi kupata taarifa muhimu kuhusu maombi yao ya vitambulisho bila usumbufu wala gharama za kufika ofisini.

Amesema kupitia mfumo huo, mwananchi ataweza kufahamu hatua iliyofikiwa katika maombi yake ya kitambulisho cha taifa, ikiwa ni pamoja na kujua kama namba ya utambulisho wa taifa imeshatolewa, kama kitambulisho kimeshachapishwa au mahali kilipo.
“Napongeza Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa kwa kuunda mfumo huu wa kisasa unaowawezesha wananchi kupata taarifa sahihi kwa haraka.
Mfumo huu ni sehemu ya jitihada za serikali kuboresha utoaji wa huduma kwa kutumia teknolojia,” amesema
Katika hatua nyingine Simbachawene aliwashukuru watoa huduma za mitandao ya simu kwa kuunga mkono juhudi za serikali kwa kukubali kuunganisha mifumo yao na mfumo wa NIDA ili kuwezesha huduma hiyo kutolewa bure kwa wananchi
.“Ushirikiano huu ni mfano bora wa namna Sekta binafsi na Taasisi za Umma zinavyoweza kushirikiana kwa maslahi ya wananchi. Mmeonyesha kwa vitendo utekelezaji wa sera ya serikali ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi,” ameongeza.

Simbachawene amesema serikali inaipongeza NIDA kwa kuendelea kuboresha huduma zake kwa kutumia teknolojia ya kisasa, akibainisha kuwa mfumo huo mpya utaondoa changamoto ya msongamano wa wananchi katika ofisi za wilaya ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama na muda wa kufuatilia vitambulisho.
Simbachawene aliwahimiza wananchi kutumia kikamilifu huduma hiyo mpya, akidai itasaidia kuondoa changamoto ya vitambulisho kubaki kwa muda mrefu katika ofisi za wilaya na kuongeza ufanisi wa huduma kwa wananchi
Kwa mujibu wa NIDA, huduma hiyo mpya inapatikana kupitia short code namba 15274, ambapo mwananchi atatuma ujumbe mfupi kwa kutumia simu ya kawaida au ya kisasa na kupata taarifa papo hapo kuhusu maombi yake ya kitambulisho cha taifa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, amesema mfumo huo umebuniwa na wataalamu wa ndani wa mamlaka hiyo, hatua iliyosaidia kuokoa fedha nyingi za serikali.
Kaji amesema mfumo huo utasaidia kupunguza malalamiko ya muda mrefu ya wananchi kuhusu ucheleweshaji wa vitambulisho pamoja na mlundikano wa watu katika ofisi za wilaya wakifuatilia taarifa zao.
Kaji alifafanua kuwa kupitia mfumo huo, mwananchi ataweza kujua kama kitambulisho chake kipo hatua gani ,kama kipo tayari, kipo wapi au kama bado kipo kwenye hatua ya uhakiki.

Pia amesema mfumo huo ,utamwezesha mwananchi kupata namba yake ya utambulisho wa taifa endapo ameisahau au kuipoteza.
Kaji amesema kwa msaada zaidi, wananchi wanashauriwa kuwasiliana na kituo cha huduma kwa wateja cha NIDA kupitia namba 0232 210500.

