Mabadiliko Makubwa Uhamiaji

Simbachawene apendekeza wasomee utalii

Agusia kigezo cha elimu ili uajiriwe Uhamiaji

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imedhamiria kuiboresha Idara ya uhamiaji ikiwa ni mpango mkakati wa kuendelea kuboresha sekta ya utalii ambayo imeliingizia taifa watalii Milioni Moja Laki Tisa Ishirini na Nne Elfu na Mia Mbili Arobaini kwa mwaka 2024 huku kwa mwaka 2025 watalii Milioni Mbili Tisini na Saba Elfu na Mia Nane Ishirini na Tatu ikiwa ni ongezeko la watalii Laki Moja Sabini na Tatu Elfu na Mia Tano Themanini na Tatu.

Akizungumza katika Kikao na Uongozi wa Juu,Maafisa Waandamizi na askari wa Idara ya Uhamiaji Visiwani Zanzibar, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,George Simbachawene amesema Maafisa Uhamiaji ni watu muhimu nchini kwa kuwa ndio watu wa kwanza mtalii au mgeni anapoingia nchini ndio anakutana nao ambapo amewataka kuwa wakarimu pindi wanapotoa huduma kwa wageni ikiwemo watalii ambao uliingizia Taifa kiasi kikubwa cha fedha ikikadiriwa Shilingi za Kitanzania Trilioni 10.14 ambapo kiasi hicho ni kwa mwaka 2024 pekee jambo linaloashiria ukuaji wa sekta ya utalii kama moja ya nguzo za Uchumi wa Tanzania.

‘Mgeni yoyote anapoingia anakutana na afisa uhamiaji, anamwambia karibu na anapoondoka anaagana nae, nyinyi ni ‘receptionist’, nyinyi ndio sura ya Tanzania, nyinyi ndio mmebeba ukarimu wetu, nyinyi ndio mmebeba utamaduni wetu, mnapaswa kuwa mfano wa kuigwa. Vyombo vingine vyote vitakapokutana na mgeni nyinyi ndio ‘expert’ wa eneo hilo, mgeni ana namna anavyokaribishwa, wako wengine wanageuza maslahi wanapomuona mgeni, na sio tu anapoingia na kutoka bali hata anapokua katika shughuli zake bado ni jukumu lenu kuhudumia wageni katika nchi yetu awe mwekezaji, mtalii nyinyi ndio jukumu lenu na mteja wenu mkubwa ni anaeingia na kutoka na hususani wageni, unapomkuta mgeni anababaishwa hata huko mitaani tafadhali sogea na ujue huyu mgeni niliemkaribisha mimi afisa uhamiaji huku mbona namuona anababaishwa, tafadhali msaidie kwasababu nyie ni wanadiplomasia namba moja mnaowakilisha mamlaka zetu za nchi.’ Alisema Waziri Simbachawene

Akizungumzia suala la vigezo vya elimu kwenye ajira za uhamiaji ili kuweza kuendana na soko la utalii, Waziri Simbachawene alisema elimu ya afisa uhamiaji hata askari wa kawaida lazima iwe diploma na kuendelea, kwasababu huyu ni mdimplomasia na anatakiwa ajue mambo mengi ikiwemo lugha fasaha ya kuongea na mtalii au mgeni anaeingia nchini.

‘Unatakiwa ujue lugha zaidi ya moja, kinyume na hapo autafika katika ngazi za hawa makamishna, wao walipita njia tofauti lakini kwa nyie vijana someni kwasababu kufika huku baadae patakua pagumu, tunataka pale anapotokea mgeni afisa uhamiaji awe anaweza kuongea kiarabu, kachina, kifaransa, kiingereza na ndio maana katika ajira tukasema lazima aanzie aliepata kiwango cha divisheni tatu kwa kidato cha nne, atafanya kazi za kawaida na awe na uwezo wa kitaaluma wa kujiendeleza lakini pia awe na uwezo wa kuwasiliana na mgeni sambamba na kujifunza masuala ya masoko ya utalii na ninaomba katika vyuo vyetu mfundishwe utalii ili mjue vivutio muwajue Wanyama.’ Aliongeza Waziri Simbachawene

Akizungumza katika kikao hicho, Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Hassan Ally Hassan amesema Idara ya uhamiaji Zanzibar inaendelea na miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa Ujenzi ya Ofisi na Makazi ya Maafisa na Askari uliopo Micheweni, Pemba Kaskazini, Ofisi ya Mkoa wa Mjini ambao ujenzi wake unaendelea,Ujenzi wa Chuo cha Uhamiaji uliopo Kitogani na Ofisi ya wilaya ya Uhamiaji iliyoko Paje.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akikagua ramani ya Ujenzi wa Ofisi ya Uhamiaji ya wilaya iliyoko Paje,Zanzibar ambapo kukamilika kwake kutasaidia uboreshaji wa huduma za kiuhamiaji,katikati ni Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Hassan Ally Hassan.Mradi huo wa Ujenzi ni ghorofa moja na umegharimu shilingi bilioni Tatu na unatarajiwa kukamilika mwisho wa mwaka huu.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akielekea ndani kukagua  Ofisi za Uhamiaji wilaya ya Kati, mkoa wa Kusini Unguja ambapo Idara ya uhamiaji imejenga ofisi hizo ili kusogeza huduma za kiuhamiaji karibu na wananchi.Katika ziara hiyo aliambatana na Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar,Hassan Ally Hassan na viongozi wa juu wa uhamiaji visiwani humo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akiteta jambo na Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar,Hassan Ally Hassan(Katikati) wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya Idara hiyo iliyojengwa sehemu mbalimbali visiwani humo ili kurahisisha huduma za kiuhamiaji kwa wananchi..Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Juu wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar,Maafisa Waandamizi na Askari baada ya kumaliza ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa visiwani Zanzibar na idara hiyo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi