Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Singida

Wananchi mkoani Singida wameipongeza Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa uboreshaji wa huduma mbalimbali , ikiwemo ya upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa ndani ya saa 48 za kazi kwa wale waliokidhi vigezo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki mkoani hapa, wakati wa uzinduzi wa kliniki ya huduma za msaada wa kisheria zinazotolewa bure, wananchi hao wamesema kuwa hatua hiyo imepunguza usumbufu, gharama na ucheleweshaji uliokuwa ukiwakabili kwa miaka mingi.

Kliniki hiyo,inayotoa huduma mbalimbali ikiwemo ile ya utatuzi wa migogoro ya ndoa, ardhi, mirathi na ukatili wa kijinsi, huduma za uwakili, huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) , RITA na elimu ya kisheria ni utekelezaji wa mpango wa serikali ya awamu ya Sita chini uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ya kusongeza huduma karibu na wananchi.

Mkazi wa Wilaya ya Manyoni, Bw. Husein Lutery amesema kupata cheti cha kuzaliwa kwa mtoto wake kulichukua chini ya siku mbili tu tangu kuwasilisha maombi, jambo alilolielezea kuwa ni hatua kubwa ya mageuzi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Nilishangaa kuona cheti kinatoka haraka hivi. Mageuzi haya katika utoaji wa huduma bora ni ya kupongezwa,” alisema Bw. Lutery.

Naye Bw. Rashid Rajabu amesema hapo awali wananchi walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo, lakini kupitia kliniki ya huduma za msaada wa Kisheria imewawezesha mwananchi kupata huduma mbalimbali katika eneo moja ikiwemo ile ya RITA.

“Vyeti vya kuzaliwa na vifo ni nyaraka muhimu sana. Kwa sasa tunavipata kwa urahisi zaidi tofauti na miaka ya nyuma. Hii imesaidia watoto wetu kuandikishwa shule kwa wakati na familia kutatua masuala ya kisheria bila usumbufu,” alisema Bw. Rajabu.

Naye Bi. Asia Rimo, kutoka kijiji cha Msisi, amesema huduma za udhamini wa mali za marehemu zinazotolewa na RITA zimepunguza migogoro ya kifamilia iliyokuwa ikijitokeza mara kwa mara. Alisema elimu inayotolewa na wakala huo juu ya masuala ya mirathi imewasaidia wananchi kuelewa taratibu sahihi za kisheria.

“Kwenye jamii zetu tumekuwa tukishuhudia migogoro mingi ya mirathi kwa sababu ya kukosa uelewa. lakini kupitia kliniki hii ambayo huduma zake zinatolewa bure, itasaidia kupunguza migogoro hiyo kwani tunapewa elimu ya namna ya kuandaa wosia na kufuata sheria,” alisema Bi. Rimo.

Kwa upande wake Meneja wa Usajili wa Vizazi, Vifo, Ndoa na Talaka kutoka RITA, Bi. Patricia Mpuya, amesema wakala imeendelea kuboresha mifumo yake ya kazi, ikiwemo kuongeza matumizi ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano (TEHAMA ) na kuwajengea uwezo watumishi wake ili kuhakikisha wananchi wanapata vyeti vya kuzaliwa ndani ya saa 48 za kazi kama ilivyopangwa.

“Tunatekeleza mpango huu kwa kuhakikisha taarifa za vizazi zinasajiliwa kwa wakati na kwa usahihi. Hii ni sehemu ya jitihada za serikali kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi,” amesema Bi. Mpuya.

Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Singida waliojitokeza kwenye uzinduzi wa kliniki ya utoaji huduma za msaada wa Kisheria (Legal Aid Clinic), wakifuatilia kwa makini hotuba ya Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Juma Homera, (hayupo pichani) uzinduzi huo ulifanyika mwishoni wa wiki katika ukumbi wa RC Mission – Mabula Stendi.

Naye Mratibu wa RITA Mkoa Singida , Bi. Devotha Mazoea amesema kupitia kliniki hiyo, maelfu ya wananchi wamejitokeza na kufanikiwa kupata huduma mbalimbali, ikiwemo huduma ya vyeti vya kuzaliwa.

“Kupitia kliniki hii, mbali ya kutoa huduma ya vyeti vya kuzaliwa, Wakala tunaendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa usajili wa vizazi na vifo, udhamini wa mali za marehemu, usimamizi wa mali za watoto pamoja na masuala ya ufilisi,: amesema Bi. Mazoea

Kliniki hiyo ya siku mbili, imekuwatanisha wadau mbalimbali wakiwemo RITA, NIDA, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mawakili wa Serikali, Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia, pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria.
Huduma hiyo ya msaada wa kisheria kwa wananchi ni endelevu katika mikoa mbalimbali hapa nchini.