Na Salma Lusangi, WMJJWW

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema kuwa imeamua kuongeza nguvu katika Programu ya Makuzi, Malezi na Maendeleo ya Awali ya mtoto (ECD) ili kuwa na jamii yenye Afya bora.

Akizungumza katika mafunzo ya siku nne kwa Waandishi wa Habari kutoka Zanzibar yaliyofanyika Agosti 5-8, 2025 katika Hoteli ya Jamirex, Dar- Es- Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Khamis Abdallah Said amesema utafiti umeonesha asilimia 18.6 ya watoto wamedumaa hivyo SMZ imeamua kuja na mbinu mpya katika Makuzi, Malezi na Maendeleo ya Awali ya mtoto.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Khamis Abdallah Said akizungumza katika mafunzo ya waandishi wa habari Zanzibar, kuhusu Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto, kushoto Mkurugenzi Mtendaji wa Muungano wa klabu za waandishi wa habari Tanzania ( UPTC) Kenethi Simbaya na kulia Meneja wa huduma za jamii katikaTaasisi ya Afisi ya Rais Ufatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikali ( PDB) Dkt Ibrahim Kabole

Amesema Programu ya ECD ipo tangu zamani lakini kwasasa Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameamua kwa makusudi programu hii iwe chini ya Taasisi ya Afisi ya Rais Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini (PDB) ndio msimamizi Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Afya.

Katibu Mkuu Khamis amesema ili Serikali iweze kupanga maendeleo lazima iwe na jamii yenye afya bora, hivyo niimani yake kwamba mafunzo hayo kwa waandishi wa Habari yataleta mabadiliko katika kuelimisha jamii, katika umuhimu wa lishe, chanjo, mtoto kunyonyeshwa miezi sita mfululizo bila kupewa chakula kingine, kutoa elimu ya jamii, ili kupunguza udumavu wa Watoto pamoja na Vifo.

Ameeleza katika kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, Tanzania imejipanga kuwa nchi yenye uchumi wa kati wa kiwango cha juu. Ili kufikia malengo hayo makubwa, imeamua kufanya mambo makubwa ikiwemo uwekezaji wa dhati katika miundombinu, rasilimali watu, n.k hivyo hatua ya kuekeza katika malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto itasidia kujenga misingi ya akili, maadili na uwezo wa uzalishaji unaohitajika katika uchumi wa kisasa.

“Serikali inafanya juhudi za makusudi za kuhakikisha watoto wote wanapata huduma bora za afya, lishe, elimu ya awali, na mazingira salama, wandishi wa Habari kupitia kalamu zenu mtaeliemisha jamii umuhimu wa ECD kwani waandishi mnauwezo mkubwa wakuleta maendeleo chanya” Alisema Said.

Mapema akizungumza katika mafunzo hayo mtaalamu wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya mtoto kutoka Taasisi ya Children Grassfire Devis Gisuka, amesema malezi na makuzi ya mtoto yanaanza tangu mtoto akiwa tumboni kwa mama hadi kufikia umri wa miaka nane (8) ikiwemo mawasiliano na lishe bora.

Naye, Muwezeshaji kutoka Madrasa Childhood Sharifa Suleiman Majid ameeleza kuwa miongoni mwa mambo yanayochangia mfumo bora wa makuzi ya mtoto ni pamoja na kuwa na afya bora, lishe, elimu ya mapema, malezi yenye uwajibikaji, ulinzi na usalama wa mtoto.

Kwa upande wake Matalaam wa Malezi na makuzi na Maendelezo ya Awali ya Mtoto kutoka UNICEF ndugu Alinune Njemwa amesema Shirika hilo litaendelea kuisaidia Tanzania katika mambo matatu (3) kukakikisha kuwa mtoto amekua katika ukamilifu wake kwa kusimamia mifumo yote ya ECD inafanyakazi, Mifumo ya Sheria na Kanuni inasimamiwa ipasavyo katika huduma za Malezi na Uwepo wa jamii Wazazi na Walezi wanatoa huduma bora.

Mafunzo hayo ya siku nne kwa Waandishi wa Habari kutoka Visiwani Zanzibar kuhusu Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto yameratibiwa na PDB kwa kushirikiana na Umoja wa Clabu ya Waandishi wa Habari Tanzania (UPTC) na kudhaminiwa na Big Win Philanthropy na UNICEF.