Na Mussa Juma, JamhuriMedia, Arusha

Jumuiya ya Wawekezaji Mahiri katika maeneo ya Wanyamapori(SOAT) imezinduliwa rasmi jijini Arusha, huku wawekezaji hao wakiahidi kushirikiana na serikali kuendeleza Utalii na kuhakikisha ndani ya miaka 20 wanaingizia taifa kiasi cha sh 790 bilioni kutokana uwekezaji wao.

Akizungumza katika Uzinduzi huo, Mtendaji mkuu wa SOAT, Erasmus Tarimo alisema wanachama wa SOAT wanatarajia kuwekeza katika miradi mbali mbali kwa jamii kwa kiasi cha USD 50 milioni kwa kipindi cha miaka ishirini sawa na shilingi bilioni 125.

Tarimo alisema kutakuwa na uwekezaji katika ulinzi wa usiopungua dola milioni 20 ili kukabiliana na majangili kwa kipindi cha miaka 20 na uwekezaji katika utafiti dola milioni 7.

Alisema SOAT, inatarajia Kuimarisha mfumo wa udhibiti ili kuhakikisha usimamizi imara na mazingira yanayotabirika ya uwekezaji wa muda mrefu unaotegemea utalii wa wanyamapori.

“ Mheshimiwa mgeni rasmi Dira yetu sisi ni kuunganisha wanyamapori, jamii na Utalii kwa ajili mafanikio endelevu ya kiuchumi na Misheni ni Kushirikiana kulinda wanyamapori, kuinua jamii katika kuhifadhi na kuendeleza utalii endelevu”alisema

Tarimo alisema, Malengo ya jumuiya hiyo kuongeza wigo wa chaguo kwa wateja kuhusiana na shughuli za matumizi na sisizo za matumizi,Kutekeleza uwekezaji bunifu kaatika utalii na kuhimiza uwekezaji mbadala na Kuendeleza na kutangaza bidhaa za utalii Pamoja na kudumisha ubora wa maeneo ya uhifadhi.

“ Pia tunakusudia Kuendeleza uwekezaji toshelezi ili kuwekeza katika kujenga miundombinu stahiki katika maeneo ya hifadhi,Kuimarisha uhifadhi , manufaa ya kijamii na kiuchumi pamoja kuzalishamapato zaidi na Kutumia rasilimali za wanyamapori kwa kutoa shughuli mbalimbali endelevu za matumizi ya wanyamapori” alisema

Akizindua umoja huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, Meja Jenerali ( Mstaafu) Hamis Semfuko alipongeza wawekezaji hao wa maeneo la Uwekezaji mahiri wa wanyamapori(SWICA) kuanzisha umoja huo ambao utasaidia sana kuimarisha mawasiliano na serikali.

Alisema tangu kuanza utaratibu wa SWICA Serikali imekuwa ikinufaika sana na uwekezaji mahiri katika maeneo ya Wanyamapori zaidi ya mara tisa kwa sasa.

Alisema Mfumo wa uwekezaji mkakati wa SWICA ulianza kutekelezwa kwa kuanzia na wawekezaji sita Kwa kiasi cha uwekezaji wenye thamani ya USD milioni 278 sawa na shilingii bilioni 696 .

Meja Generali mstaafu , Semfuko alisema awali SWICA ilikuwa na wawekezaji sita na sasa kuna wawekezaji 13 na wapo wengine ambao wanataka kuwekeza hatua ambayo inaonesha umuhimu wa uwekezaji huu mahiri katika sekta ya Utalii.

Alisema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akifatilia sana uwekezaji katika SWICA na anaamini kuwa unakwenda kulinufaisha sana Taifa lakini pia kuchangia kupunguza migogoro baina ya wanyamapori na binaadamu na kuongeza ajira na mapato.

Awali Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori(TAWA), Mlage Yussuf Kabange alisema alisema maeneo ya SWICA yapo ndani ya maeneo ya TAWA hivyo,SOAT itapewa ushirikiano mkubwa kuhakikisha inafikia malengo yake.

Kamishna Kabange alisema alisema TAWA inaamini kukiimarishwa ushirikiano, lengo la Serikali kufikisha watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030 litafanikiwa.

Akizungumza Kwa niaba ya Mwenyekiti wa SOAT, Makamu Mwenyekiti Martha Lucumay alisema wamejipanga kufanyakazi na serikali lakini wanaomba pia changamoto kadha ikiwepo za kikodi kufanyiwa kazi

Akizungumza katika uzinduzi huo,Mmoja wa Wakurugenzi wa kampuni ya Mwiba Holdings Ltd ambayo ni miongoni mwa wanachama waanzishilishi wa SOAT.Nicolaus Negri alishukuru Serikali kufika katika uzinduzi huo na kuahidi SOAT itafanyakazi kwa kushirikiana na Serikali.

Negri pia aliewashukuru viongozi wa chama cha mawakala wa Utalii nchini(TATO) chama cha Wawindaji wa Utalii nchini(TAHOA), Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori(TAWIRI) na wadau wengine wa Utalii kushiriki katika uzinduzi huo amba oni muhimu katika kuboresha sekta ya uhifadhi na Utalii nchini.

Maeneo ambayo yanawekezwa kupitia SWICA ni Eneo la kaskazini la pori la akiba la Maswa,Maswa Kimali ,Maswa Mbono;Mapori ya akiba ya Grumeti na Ikorongo;.Pori la akiba la Mkungunero,Pori Tengefu la Ziwa Natroni na Kitalu cha LL1 katika pori la akiba la Selous.