Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, amesema Bunge litaendelea kuishauri na kuisimamia Serikali kushughulikia kwa haraka changamoto ya ucheleweshaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, huku akisisitiza kuwa elimu ni kipaumbele katika ajenda ya maendeleo ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Akizungumza kwenye Mahafali ya nane ya Seneti ya Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Tulia amesema kuwa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu, na kwamba Bunge litaendelea kulifuatilia suala la utoshelevu wa mikopo ili kuhakikisha wanafunzi wote wenye uhitaji wanapata huduma hiyo kwa wakati.

“Tutaendelea kuishauri Serikali pamoja na Waziri wa Elimu ili kuhakikisha changamoto ya ucheleweshwaji wa mikopo inapatiwa ufumbuzi wa kudumu,” alisema Dkt. Tulia.

Aidha, amesisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinawathamini wasomi na kila mmoja ndani ya jamii, na kwamba maoni ya wananchi, hasa vijana, yamekuwa yakizingatiwa na kufanyiwa kazi na chama hicho tawala.

“Tunaenda na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu maeneo mengi ameyawezesha, hususan katika elimu. Ni CCM pekee yenye uwezo wa kusogeza maendeleo haya mbele zaidi. Oktoba nenda ukapige kura, mchague Samia na viongozi wengine wa CCM,” ameongeza.

Dkt. Tulia pia ametumia jukwaa hilo kuwahamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika siasa, uchaguzi, na maendeleo ya nchi.

Amesema Serikali inajipanga kuanzisha mitaa ya viwanda katika kila halmashauri ili kuibua ajira na fursa zaidi kwa vijana.

“Mageuzi ya kiuchumi yanategemea vijana. Rais Samia anataka kuona kila kijana mwenye uwezo anapata nafasi ya ajira au kujishughulisha na shughuli za maendeleo. Tusiogope kugombea nafasi za uongozi. Fursa zipo – muhimu ni maandalizi,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Nasra Ramadhani, amesema Mkoa uko salama kisiasa na vijana wameshiriki kikamilifu katika michakato yote ya uchaguzi ikiwemo uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

“Tunayo mahusiano mazuri kati ya chama, taasisi za elimu ya juu na halmashauri zetu. Kupitia asilimia 10 za mapato ya ndani, vijana wamewezeshwa kiuchumi,” amesema.

Amewataka vijana wenye sifa kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ifikapo Juni 18 na kushiriki uchaguzi kwa bidii.

Muhitimu Maria Mapunda amesema Serikali imewasaidia sana, hasa katika ongezeko la mikopo na utekelezaji wa mradi wa HEET ulioleta mabadiliko makubwa vyuoni.

“Sisi wasomi tukishindwa kusaidia taifa, nani atasaidia? Tuende tukamtangaze Rais Samia na kulinda amani iliyopo,” amesema.

Akichangia kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema mfumo wa “KKK – Kula, Kulala, Kusoma” umeongezewa maana kwa kuongeza “Kusoma kwa bidii huku ukifanya kazi”, akibainisha kuwa viwanda vitaanza kuchukua wanafunzi kama hitaji la kisheria.

“CCM imetambua kuwa ajira bado ni changamoto, ndiyo maana tumepanga kila mtaa uwe na viwanda,” amesema Profesa Mkumbo.