Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, amesema hadi sasa Ofisi ya Spika haijapokea taarifa yoyote ya wito wala kutoa kibali cha mbunge yeyote kwenda kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Spika Zungu amesema ametoa ufafanuzi huo kufuatia taarifa zilizosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari zikidai kuwa baadhi ya wabunge wameitwa kuhojiwa na TAKUKURU kuhusiana na madai waliyoyatoa wakati wakichangia mjadala wa hotuba ya Rais Bungeni.
Akizungumza leo Februari 5,2026 amesema Bunge linaongozwa na Katiba na Kanuni zake, ambazo zinawalinda wabunge kutoa maoni yao kwa uhuru bila shinikizo, hofu, kuhojiwa, kushtakiwa au kikwazo chochote kinachoweza kuathiri utekelezaji wa majukumu yao ya kikatiba.
Kwa mujibu wa Spika, uhuru huo wa wabunge umeainishwa na kulindwa chini ya Ibara ya 100 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayowapa wabunge kinga ya kisheria kwa maoni na michango wanayoitoa ndani ya Bunge.
Ameeleza kuwa endapo itatokea mbunge amekiuka Kanuni za Bunge wakati wa mjadala au katika mchango wake, mamlaka ya kuchukua hatua yapo ndani ya Bunge lenyewe kupitia Kiti cha Spika, ikiwemo kufuta mchango husika kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Spika Zungu amesema Kanuni za Kudumu za Bunge la mwaka 2025, hususan Kanuni ya 5, zimeweka bayana namna ya kushughulikia ukiukwaji wowote unaotokea ndani ya Bunge, bila kuingilia uhuru wa mbunge au kuvunja misingi ya kinga ya kibunge.
Amesisitiza kuwa Bunge litaendelea kulinda uhuru wa wabunge kuchangia masuala ya kitaifa kwa uwazi na ujasiri, huku likihakikisha mijadala inafanyika kwa kuzingatia kanuni, heshima na misingi ya kikatiba.


