Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

KURA za maoni kwa watia nia wa ubunge na udiwani ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata na Majimbo yote ya uchaguzi hapa nchini zimehitimishwa jana na kushuhudiwa damu mpya zikipenya katika uchaguzi huo.

Akizungumza na gazeti hili leo, Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora Idd Moshi ameeleza kuwa zoezi hilo limefanyika kwa amani na utulivu katika Wilaya zote za Mkoa huo.

Amebainisha kuwa katika Majimbo yote kumi na mbili (12) ya ubunge yaliyopo katika Mkoa huo ni majimbo mawili tu ambayo wabunge wanaomaliza muda wao wamepata ushindi katika hatua hii ya kura za maoni, wengine wote wamepigwa.

Ametaja majimbo 2 ambayo wabunge wa zamani wamepeta kuwa ni Urambo (Magreth Simwanza Sitta) na Nzega Mjini (Hussein Mohamed Bashe) huku majimbo 10 yaliyobaki walioshinda kura za maoni ni damu mpya.

Ametaja walioibuka kidedea katika jimbo la Tabora Mjini ni Shabani Zuberi Mrutu, Uyui (Shaffin Ahmeda Sumar), Sikonge (Munde Abdallah Tamwe), Kaliua (Denis Longino Kilatu) na Bukene (John Stephano Luhende).

Majimbo mengine ni Nzega Vijijini (Neto Paul Kapalata), Manonga ( Abubakar Ally Omari), Igunga Mjini (Henry Charles Kabeho), Igalula (Juma Mustafa Ramadhan Kawambwa) na Ulyankulu-Kaliua ( Japhael Masanja Lufungija).

Katibu wa Siasa na Uenezi amefafanua kuwa haya ni matokeo ya awali ambayo yatapelekwa katika vikao vya ngazi za juu vya chama kwa ajili ya uteuzi wa mwisho, aliwataka wagombea wote kuwa watulivu na kusubiri uamuzi wa vikao.

Amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama katika ngazi za kata kwa kufanya maamuzi yao kupitia karatasi za kura kwa watia nia ya ubunge na udiwani katika maeneo yao.

Akiongea kwa niaba ya watia nia wenzake Shabani Mrutu amepongeza Uongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi kwa kuweka utaratibu mzuri wa kutambulishwa wagombea katika kila kata na kisha kupigiwa kura ya diwani na mbunge.

‘Huu utaratibu ni mzuri sana, unawapunguzia gharama za kusafiri kwenda Makao Makuu ya Wilaya wajumbe, ndiyo maana wamepiga kura kwa amani na utulivu na kupata watu sahihi wanaowataka wenyewe’, ameeleza.