Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, amezitaka taasisi zote za umma kufanya mapitio ya sera, sheria na kanuni zinazokinzana ili kuweka mazingira bora ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025.

Dkt. Nchemba ametoa kauli hiyo wakati akizindua sera hiyo kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa mabadiliko ya kimfumo ni muhimu katika kuondoa vikwazo vinavyokwamisha ufanisi wa sekta ya ununuzi wa umma.

Amesema changamoto nyingi zinazoikabili sekta hiyo hazitokani na upungufu wa sera au sheria, bali uzembe na mitazamo ya baadhi ya watendaji, huku akirejea taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) zinazoonesha utekelezaji dhaifu wa taratibu zilizopo.

“Ni lazima tubadili mtazamo na kuwajibika ipasavyo ili kufikia malengo ya sera hii,” amesisitiza Dkt. Nchemba.

Katika hatua nyingine, Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imesema ujenzi wa moduli ya kisasa ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa kupitia mfumo wa NeST ni hatua muhimu itakayoongeza uwajibikaji, uwazi na ufanisi katika mnyororo wa ugavi nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando, amesema moduli hiyo imeunganisha wazabuni wote na taasisi nunuzi nchini, hatua itakayorahisisha utatuzi wa migogoro inayotokana na michakato ya ununuzi wa umma.

Ameeleza kuwa matumizi ya mfumo huo yatasaidia kufanya maamuzi kwa haki na kwa wakati, kupunguza gharama za uendeshaji, kuokoa muda na kuboresha utunzaji wa kumbukumbu, hivyo kuongeza ufanisi wa miradi ya Serikali.

Aidha, amesema PPAA imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha mifumo ya ugavi kupitia ushiriki wake katika utungwaji wa sera, sheria na kanuni mbalimbali za ununuzi wa umma, hatua inayolenga kuongeza uwazi na nidhamu katika matumizi ya fedha za umma.

Katika kuboresha zaidi upatikanaji wa haki,amesema mamlaka hiyo inapanga kuweka mazingira rafiki kwa makundi maalum ikiwemo vijana, kwa kupunguza gharama za mashauri na kuongeza uelewa wao kuhusu fursa zilizopo katika mfumo wa ununuzi wa umma.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar, amesema sera hiyo ni mwongozo muhimu utakaosaidia kuimarisha mifumo ya ugavi, kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma na kudhibiti vitendo vya rushwa.

Ameongeza kuwa utekelezaji wake utafungua fursa za ajira, kuimarisha mnyororo wa thamani na kuchochea mageuzi makubwa ya kiuchumi kuelekea dira ya maendeleo ya mwaka 2050.