Juni 10, 2025 katika Mahakama ya Wilaya Tarime mbele ya Mheshimiwa Veronica Seleman (Hakimu Mfawidhi) wa mahakama hiyo, imefunguliwa kesi ya Rushwa Namba 13960/2025 – Jamhuri dhidi ya JACOB IBRAHIM WANKYO, Tabibu wa Kituo cha Afya Magena.

Akisoma hati ya mashtaka, Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Bw. William Lyamboko amesema, mshtakiwa huyo anashtakiwa kwa kosa la kuomba hongo ya shilingi 350,000/- na kupokea hongo ya shilingi 200,000/-, kosa chini ya kifungu cha 15(1)(a) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Pitio la 2022.

Bw. Wiliam Lyamboko alieleza kuwa, mshtakiwa huyo aliomba rushwa kwa mgonjwa aliyekuwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa uzazi hivyo kuomba rushwa ili aweze kumpatia huduma hiyo ya upasuaji katika kituo hicho cha afya.

Hata hivyo, baada ya mshtakiwa kusomewa Hati ya Mashtaka amekana makosa yake.

Mshtakiwa amepata dhamana baada ya kutimiza masharti ya mahakama ambayo alitakiwa kuwa na wadhamini wawili ambapo kila mmoja alitakiwa kusaini fungu la dhamana ya Tsh. 4,000,000.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 26.06.2025 itakapokuja kwa ajili ya kusomwa kwa hoja za awali.