RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kutoa zawadi ya sh bilioni moja kwa timu ya taifa ya soka, Taifa Stars, iwapo itatwaa ubingwa wa michuano ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2024 inayopangwa kuanza Agosti 2 hadi 30 ikiandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Julai 24, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi, amesema donge hilo ni motisha na kwamba ana imani Taifa Stars italipambania Taifa kwa jasho na damu na kupeperusha vyema bendera ya nchi.

“Iwapo Taifa Stars itafanikiwa kutwaa ubingwa wa CHAN 2024, Serikali itatoa zawadi ya shs bilioni moja, lakini ikifika fainali itavuna sh milioni 500, wakifika nusu fainali watapata sh milioni 200 lakini pia, kutakuwa na goli la Mama ambapo kwenye hatua ya nusu fainali goli litakalofungwa ni sh milioni 20,” amesema Prof. Kabudi.

Kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa, kila goli litakalofungwa na Taifa Stars katika hatua ya makundi, timu itazawadiwa sh milioni 10.

Msigwa pia ametoa wito kwa vyombo vya habari, wasanii, na mashabiki wote kuungana katika kampeni ya kitaifa ya kuiunga mkono Stars kuelekea CHAN 2024.

Katika hatua nyingine, Waziri Kabudi ameeleza kuwa maandalizi ya miundombinu kwa ajili ya mashindano hayo yako katika hatua ya mwisho, huku viwanja vya Benjamin Mkapa na Azam Complex vikikaguliwa na kuthibitishwa na wataalamu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mchezo wa ufunguzi ambapo Taifa Stars itachuana na Burkina Faso Agosti 2, 2025 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku mgeni rasmi akiwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Waziri Kabudi amesema mafanikio ya maandalizi yametokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali kwa kutoa kipaumbele katika kuboresha miundombinu ya michezo, huduma za kijamii, viwanja vya mazoezi, pamoja na malazi, usafiri na huduma za afya kwa timu zote shiriki.

Serikali imetangaza pia, mpango wa uhamasishaji mkubwa, ikiwemo kuandaa tamasha kubwa la CHAN Singeli litakalofanyika kwa siku mbili mfululizo kuashiria uzinduzi wa mashindano hayo.

Ili kuhakikisha Watanzania wengi wanapata fursa ya kushiriki mashindano haya, Serikali imetangaza viingilio rafiki – kuanzia Sh 2,000 kwa mzunguko, Sh 5,000 kwa VIP B, na Sh 10,000 kwa VIP A.

“Nitumie fursa hii kuwaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kushangilia timu yetu na kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi na kibiashara zitakazokuja na mashindano haya,” amesema Prof. Kabudi.