TAKRIBAN watu 55 wakiwemo watoto wameuawa usiku wa kuamkia Jumanne na vikosi vya Israel katika Ukanda wa Gaza.

Miongoni mwa waliouawa walikuwemo watu 15 waliokuwa wakisubiri msaada wa kibinaadamu katika kivuko cha Zikim kaskazini mwa Gaza.

Wizara ya Afya ya Gaza imetahadharisha kuwa hali ya kibinaadamu inazidi kuwa mbaya eneo hilo ambapo Wapalestina wengine watano, ikiwa ni pamoja na mtoto, wamekufa kwa utapiamlo katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Hayo yanajiri wakati Israel imeendelea kukosolewa kufuatia mauaji ya mwanahabari wa Al-Jazeera Anas al-Sharif na wafanyakazi wengine wa shirika hilo la utangazaji.

Umoja wa Ulaya umelaani mauaji hayo na kuitaka Israel kuwasilisha ushahidi uliowazi kwamba wanahabari hao walikuwa magaidi kama ilivyodai, ili kuepusha kitendo hicho kisijirudie.