Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Lindi imetoa taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu yake kupitia programu ya TAKUKURU Rafiki, ikibainisha kuwa imefanikiwa kutatua kero mbalimbali zilizowasilishwa na wananchi, hususan kwenye sekta za elimu, afya, maji, nishati na utawala.
Katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2025, TAKUKURU Lindi imepokea malalamiko 52, ambapo 44 yanahusu rushwa na manane hayahusiani na rushwa. Mashauri manne yalifikishwa mahakamani na watuhumiwa wote walitiwa hatiani.
Aidha, taasisi hiyo imesema kuelekea Uchaguzi Mkuu inatarajia kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa, kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu thamani ya kura, madhara ya rushwa na umuhimu wa kuchagua viongozi bora.
Vilevile, imejipanga kuimarisha ufuatiliaji wa manunuzi ya umma, utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kuchukua hatua kali dhidi ya wale wote watakaobainika kufuja mali za umma.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Lindi, Stephen Mafipa, amewashukuru wananchi, vyombo vya habari na taasisi mbalimbali kwa ushirikiano wao katika mapambano dhidi ya rushwa.
“Ninawaomba wananchi na wadau wote waendelee kutuunga mkono kwa kuzuia vitendo vya rushwa visitokee, kwani kuzuia rushwa ni jukumu la kila mmoja wetu,” alisema Mafipa.
Kauli mbiu ya TAKUKURU Mkoa wa Lindi imeendelea kusisitizwa kuwa: “Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu, Tutimize Wajibu Wetu.”
