Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Tabora imenasa jumla ya wafanyabiashara 7 waliokuwa wakiuza mali za wizi za wakulima wa zao la tumbaku zenye thamani ya sh bil 1.4.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani hapa Azza Mtaita amethibitisha kukamatwa watuhumiwa hao alipokuwa akiongea na waandishi wa habari Ofisini kwake jana na kueleza kuwa wafanyabiashara hao wamekamatwa katika operesheni maalumu.
Amebainisha mali zilizokamatwa kuwa ni mabelo ya magunia ya kufungashia zao hilo yajulikanayo kama majafafa ambayo ni mali halali ya wakulima, jumla ya magunia 2,681 yenye thamani ya sh bil 1.4 yamekamatwa katika maeneo tofauti.

Kamanda Mtaita amefafanua kuwa magunia hayo yamekamatwa kutoka kwa wafanyabiashara baada ya kukutwa wakiyauza kinyume na taratibu huku wakijua fika kuwa ni mali halali ya wakulima kwa sababu waliyanunua msimu uliopita.
Amedokeza kuwa wote waliokamatwa walifikishwa mahakamani ili kujibu tuhuma zinazowakabili, lakini akabainisha kuwa wakati kesi ikiendelea baadhi yao waliomba kufanya makubaliano (pre bargaining) ya kulipa fidia ya hasara.
‘Utaratibu huu wa makubaliano (plea bargaining) ya kulipa fidia ya hasara kwa wakulima umesaidia kuokoa kiasi cha sh mil 2 na kurejeshewa magunia yao ili wayatumie kufungashia tumbaku yao msimu ujao’, ameeleza.
Amebainisha kuwa baada ya makubalinao hayo na kulipwa fidia ya hasara kwa serikali, walifanikiwa kurejesha jumla ya magunia 1,315 yaliyotumika msimu uliopita kati ya 2,681 yaliyokamatwa.

‘Wakulima wanaponunua magunia ya kufungashia tumbaku yanakuwa mali yao, kampuni yoyote inayoingia mkataba wa kununua tumbaku inapaswa kuyarejesha kwa wakulima ili yatumike msimu mwingine na sio kuwauzia tena’, ameasa.
Kamanda Mtaita ametaja wakulima waliorejeshewa magunia hayo kuwa ni wa kutoka vyama vya msingi (Amcos) za Mulokhu, Mkombozi, Ikobelo na Kasisi, taratibu za ufuatiliaji zinaendelea ili kuhakikisha magunia yaliyosalia yanarejeshwa kwa wakulima kupitia vyama vyao vya msingi.