Na Mwandishi Wetu, Indaba, Afrika Kusini

Chama cha Wasambazaji wa Bidhaa na Watoa Huduma Migodini (TAMISA) kinashiriki katika Kongamano la Kimataifa la Madini ( Mining Indaba 2026) linaloendelea jijini Cape Town, Afrika Kusini, kwa lengo la kuendeleza na kuimarisha sekta hiyo duniani. Ushiriki huo wa TAMISA ni sehemu ya ujumbe wa wadau wa sekta ya madini kutoka Tanzania unaoongozwa na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde.

Akizungumza, Mwenyekiti wa TAMISA, Bw. Peter Kumalilwa, amesema mkutano huo una umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya sekta ya madini nchini, kwani unatoa fursa kwa TAMISA kutambua na kuchangamkia maeneo mapya ya uwekezaji na ushirikiano wa kibiashara.

“Tunapata fursa ya kujifunza namna biashara ya madini inavyoendeshwa barani Afrika na duniani kwa ujumla,” amesema Bw. Kumalilwa.

Ameongeza kuwa kupitia kongamano hilo, TAMISA inalenga kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini, sambamba na kuvutia uwekezaji utakaowanufaisha wazawa kupitia utekelezaji wa Sheria ya Maudhui ya Ndani (Local Content).

Akiwa katika mkutano huo, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde alifanya vikao vya pembeni na wadau mbalimbali, ikiwemo Benki ya Dunia, pamoja na kushiriki Mkutano wa Mawaziri wa Madini wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Katika mazungumzo hayo, Benki ya Dunia iliipongeza Tanzania chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa za kukuza uchumi wa taifa kupitia sekta hiyo na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji.

Benki hiyo pia iliunga mkono juhudi za kuimarisha tafiti za jiosayansi na kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi badala ya kusafirisha malighafi, hatua inayolenga kuongeza ajira, mapato ya Serikali na manufaa mapana ya kiuchumi kwa Watanzania.

Aidha, Naibu Balozi wa Australia nchini, Bw. Christopher Ellinger, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazopewa kipaumbele na kampuni za Australia katika uwekezaji wa sekta ya madini. Ameeleza utayari wa nchi hiyo kushirikiana na Tanzania kuendeleza miradi ya madini, huku akiomba ufafanuzi kuhusu kanuni za ushirikishwaji wa Watanzania katika utoaji wa huduma migodini.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde alikutana na kampuni ya Faru Graphite, inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Black Rock Mining, inayotarajia kuendeleza mradi wa madini ya kinywe katika eneo la Mahenge, wilayani Ulanga mkoani Morogoro. Kampuni hiyo imeripoti maendeleo mazuri ya maandalizi ya mradi na kuishukuru Serikali kwa ushirikiano wake.

Vilevile, kampuni ya Plantcor Mining ya Afrika Kusini ipo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba wa ubia na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa ajili ya kuendeleza mradi wa uchimbaji dhahabu katika eneo la Kigosi, mkoani Geita.

Kupitia ushiriki wake katika Mining Indaba 2026, Tanzania imeendelea kujiimarisha kimataifa kama kitovu cha uwekezaji katika sekta ya madini, huku jitihada za Serikali na wadau zikilenga kuhakikisha rasilimali za madini zinachangia kikamilifu maendeleo ya uchumi wa taifa na ustawi wa wananchi.

Mwenyekiti wa Chama cha Wasambazaji wa Bidhaa na Watoa Huduma Migodini ( TAMISA) Bw. PETER kumalilwa akiwa katika kongamano la Kimataifa la Madini linaloendelea Afrika Kusini