Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Chama cha Wasambazaji wa Bidhaa na Watoa Huduma Migodini (TAMISA) kimewataka vijana na Watanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya madini kwa kutumia mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni tano inayotolewa na Serikali kwa ajili ya kuwawezesha kupata mitaji ya kusambaza bidhaa na kutoa huduma mbalimbali migodini.

Rai hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa TAMISA, Bw. Peter Kumalilwa, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu fursa lukuki zinazopatikana katika sekta ya madini, akisisitiza umuhimu wa Watanzania kuzitumia kikamilifu kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Bw. Kumalilwa alisema kuwa katika jitihada za kuongeza ajira na kukuza uchumi kupitia sekta ya madini, Serikali imetenga kiasi cha shilingi trilioni tano kwa ajili ya kuwawezesha Watanzania wanaojihusisha na shughuli za usambazaji wa bidhaa na utoaji wa huduma katika migodi mbalimbali nchini.

“Kwa muda mrefu hakukuwa na mwamko wa kutosha wa kutumia mikopo hiyo, lakini tangu TAMISA ilipoanza kutoa elimu kwa wasambazaji wa bidhaa na watoa huduma migodini, mwamko umeongezeka kwa kiasi kikubwa,” alisema Bw. Kumalilwa.

Aidha, aliwataka wadau wote wa sekta ya madini kujiunga na TAMISA ili waweze kupata taarifa sahihi, fursa na mafunzo yatakayowawezesha kuongeza ufanisi, ushindani na tija katika shughuli zao za kiuchumi.

Bw. Kumalilwa aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa kipaumbele kikubwa kwa sekta ya madini, hususan kwa kuhakikisha wazawa wanapata nafasi stahiki katika usambazaji wa bidhaa na utoaji wa huduma migodini, kwa kuzingatia sera na sheria ya maudhui ya wazawa (Local Content).

Alifafanua kuwa sekta ya madini kwa sasa inachangia zaidi ya asilimia 10 ya Pato la Taifa (GDP), huku Serikali ikitangaza fursa 20 maalum kwa wazawa kwa lengo la kuwasaidia kuhama kutoka kwenye usambazaji wa bidhaa na kuelekea kwenye uzalishaji wa bidhaa hizo.

Baadhi ya fursa hizo ni pamoja na utengenezaji wa vifaa vya ujenzi kama saruji, nondo na nyaya, uzalishaji wa vilainishi mbalimbali, utengenezaji wa vilipuzi vya miamba, huduma za kisheria pamoja na huduma za usafirishaji wa mizigo na shehena.

“Watanzania, hususan vijana, watapewa kipaumbele katika utoaji wa huduma hizi migodini, hivyo tunawaomba wajitokeze kwa wingi kuchangamkia fursa hizi,” alisema Bw. Kumalilwa.


Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa TAMISA, Bw. Japhet Mussa, alisema Serikali inatambua dhamira ya dhati ya Watanzania wengi ya kushiriki kikamilifu katika biashara ya madini na iko tayari kuunga mkono jitihada hizo ili kuongeza ushiriki wa wazawa katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.


“Tunahimiza Watanzania kuwekeza katika sekta ya madini kwa kuwa TAMISA imepewa na Serikali ekari 125 zilizopo eneo la Buzwagi, mkoani Shinyanga, kwa ajili ya wawekezaji wa ndani kujenga viwanda vitakavyozalisha bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kuhudumia soko la madini,” alisema Bw. Mussa.

Aliongeza kuwa TAMISA, kwa kushirikiana na Serikali, iko tayari kulinda soko la bidhaa za wawekezaji wa ndani, akibainisha kuwa hata sheria za uwekezaji zinatoa ulinzi wa kutosha. Hivyo aliwataka Watanzania wenye mitaji kutumia fursa hiyo adhimu kutokana na uhakika wa soko uliopo katika sekta ya madini.