Na Jacob Kasiri, Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amelipongeza na kusema kuwa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limepiga hatua makubwa kuja kushiriki maonesho hayo ya kimataifa ya biashara ili kutangaza vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji zinazopatikana katika maeneo hayo adhimu na ya kimkakati nchini.
Alitanabaisha hayo leo Januari 07, 2026 alipotembelea Banda la TANAPA wanaoshiriki Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar (ZITF) ikiwa ni shamra shamra za kuelekea miaka 62 ya Sikukuu ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964, maonesho yanayofanyika katika Viwanja vya Dimani – Fumba, mjini Magharibi Zanzibar.

Aidha, wakati akizindua rasmi maonesho hayo leo, Mhe. Abdulla alipigilia msumari kwa kusema, “Nitumie fursa hii kuwahamasisha watanzania wote kutembelea vivutio vya utalii ili muvishuhudie na baadaye kuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania ndani na nje ya Tanzania.”
Naye, Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini, Naibu Kamishna wa Uhifadhi Steria Ndaga, akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais katika Banda la TANAPA kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi alisema;
“Kwa TANAPA, maonesho haya ni fursa nzuri ya kujitangaza kwani washiriki wanaoshiriki maonesho hayo ni wengi ikijumuisha watanzania na wengine ni kutoka maitaifa tisa ambayo ni Brazil, Oman, Uganda, Misri, Congo na Zambia, hii kwetu ni mtaji na ni nadra kwa mataifa kama haya kukusanyika kwa wakati mmoja isipokuwa katika mikusanyiko ya kibiashara kama hii.”

Sanjari na hilo pia katika maonesho haya, TANAPA itakuwa na ziara za kuwatembelea wadau mbalimbali wa sekta ya utalii na kujadiliana nao namna nzuri ya kuunganisha vifurushi vya utalii wa fukwe unaofanyika Zanzibar na ule wa kutembelea nyikani ili kuona wanyamapori, maporomoko ya maji na mandhari nzuri za Hifadhi za Taifa, alidadavua Kamishna Ndaga.
Vile vile, Kamishna Ndaga aliongeza kuwa Zanzibar ni soko la kimkakati kwa Hifadhi za Taifa Mikumi na Nyerere. Mathalani, kwa siku tunapokea takribani ndege kumi na watalii zaidi ya 200 katika Hifadhi ya Taifa Mikumi wakitokea Zanzibar, hivyo lengo la mkakati wa kuwatembelea wadau wa utalii na usafirishaji anga ni pamoja na kupanua wigo wa safari na kuzifikia hifadhi kama Katavi, Ruaha, Mahale na Kitulo.
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) linalosimamia maliasili zote zilizomo ndani ya Hifadhi za Taifa 21, wapo visiwani Zanzibar kunadi vivutio vyake, kutoa elimu ya uhifadhi na kuhamasisha wawekezaji kuwekeza katika maeneo hayo yenye tunu za Taifa.





