Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
Wananchi wanasisitizwa kufichua wahalifu wanaohujumu miundombinu ya umeme (TANESCO),ikiwa ni pamoja na wanaoiba transfoma, nyaya na kuchezea mita, na yeyote atakayefichua watu hao atapatiwa donge nono kuanzia sh. 100,000 hadi sh. 1,000,000.
Ofisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja kutoka TANESCO mkoa wa Pwani, Esther Msaki, alieleza hayo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki mjini Kibaha.
Alieleza vitendo hivyo, vimekuwa vikisababisha hasara kubwa kwa shirika, huku baadhi ya maeneo yakikosa huduma ya umeme kwa muda mrefu kutokana na uharibifu huo.
“Tunaomba ushirikiano wa wananchi, Yeyote atakayetoa taarifa sahihi kuhusu hujuma hizi atalipwa zawadi ya fedha taslimu kuanzia Sh .100,000 hadi Sh. milioni moja, kulingana na ukubwa wa taarifa atakayotoa,” alieleza Msaki.

Alifafanua kuwa, baadhi ya maeneo yamekuwa na matukio ya wizi wa transfoma, nyaya na vifaa vingine vya umeme, jambo linalosababisha shirika kutumia rasilimali nyingi kurejesha huduma na kuongeza gharama za uendeshaji.
Aidha, Msaki alihimiza wananchi wanaotaka kununua nyumba au viwanja kuhakikisha wanapata taarifa rasmi kutoka TANESCO ili kujiridhisha kama eneo hilo halina madeni ya nyuma kabla ya kufanikisha ununuzi.
“Tumeona baadhi ya wananchi wakiingia kwenye usumbufu kwa kununua nyumba zenye madeni ya zamani ya umeme,”,
Vilevile shirika hilo linawahamasisha wateja wanaodaiwa madeni ya nyuma yenye riba kufika ofisi za TANESCO kwa ajili ya kupata msamaha wa riba huku wakiendelea kulipa deni halisi.
“Huu ni mpango wa kusaidia wateja warejee katika huduma kwa utaratibu usiowaumiza, hata wale wenye madeni ya muda mrefu wanakaribishwa kwa mazungumzo,” alieleza Esther.

Kwa mujibu wa Ofisa Uhusiano huyo Tanesco mkoani Pwani, TANESCO kwa kupitia Wizara ya Nishati, inahamasisha matumizi ya nishati safi, ikiwemo majiko janja, ambayo hutumia umeme kidogo na ni salama kwa mazingira.
“Kwa mfano, unaweza kupika maharage kwa dakika 40 kwa kutumia unit moja ya umeme kwa Sh .350 , Ikilinganishwa na kopo la mkaa wa Sh .2,000 ambalo linaweza kuisha kabla hata chakula kuiva,”
Esther aliwataka wananchi kuunga mkono juhudi za serikali na TANESCO katika kulinda miundombinu ya umma, kutumia nishati safi na kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana kwa ufanisi na usalama.
