Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Ruvuma limeanzisha mpango wa kuwakopesha majiko wateja wapya wanaounganishia umeme na kufanya marejesho kupitia mfumo wa malipo ya LUKU ili kuwapa fursa ya kutumia nishati safi ya umeme.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo Afisa uhusiano na huduma kwa wateja Lucia Renatus amesema kuwa zoezi hilo kwa Mkoa wa Ruvuma limeanza rasmi Leo Oktoba 17/2025 Ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha maisha ya wananchi na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya Kupikia ya umeme.

Alisema kuwa wanakopesha majiko hayo kwa sababu wanahitaji Jamii itumie matumizi safi ya nishati kwa kutumia umeme hivyo majiko hayo watayalipia kidogo kidogo ndani ya miezi 6 kwa muda mwaka Mmoja kulingana na uwezo wa mteja.

” Kama tunavyojuwa kampeni ya mama Samia ya kupika kwa kutumia nishati safi ya kupikia na kuondokana na nishati zingine za kupikia sisi Tanesco kama mnavyojuwa tunapika kwa kutumia nishati safi ya umeme kwa hiyo malengo yetu ni kwamba ifikapo 2030 anayosema Rais wa Jamuhuri ya Muungano Dk. Samia watu wote tutumie umeme kupikia kwa sababu ni nishati nafuu kuliko nishati zote za kupikia” alisema Afisa uhusiano na huduma kwa wateja Renatus.

Aidha alibainisha tofauti iliyopo kati ya Mkaa na nishati ya umeme ni kwamba gharama ya nishati ya Mkaa ni kubwa kuliko umeme ambapo umeme unaweza kutumia unit 1 ni sh. 292 bila VAT kwa hiyo unit moja unaweza kupika siku nzima kwa bei hiyo ukilinganisha na bei ya Mkaa wa sh. 1000 au 2000.

Kwa upande wao baadhi ya wateja waliounganishiwa huduma ya umeme katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wameipongeza Serikali kupitia shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kuanzisha zoezi hilo ambalo litasaidia kupunguza gharama za kutumia nishati ya Mkaa na kuharibu mazingira.

Said Shaibu mkazi wa mtaa wa majengo kata ya Majengo Manispaa ya Songea alisema kuwa zoezi hilo amelipokea kwa furahaa kubwa kwani huduma hiyo ya majiko ya nishati safi ya kupikia inaendana na wakati na kwamba hiyo iwe chachu kwa watu wengine ambao hajaunganishiwa majiko hayo.