Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Nyasa
Baadhi ya wananchi mkoani Ruvuma wameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuanzisha mpango wa kuwakopesha majiko sanifu yenye presha, ambayo yanatumia umeme kwa ufanisi mkubwa na kwa gharama nafuu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo kwenye Kampeni ya Unganisha Umeme,Pika kwa Umeme na umeme ni nishati nafuu zaidi jikoni,baadhi ya wananchi wamesema kuwa majiko hayo yataleta mabadiliko makubwa katika maisha yao ya kila siku, hasa kwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, hivyo kusaidia kuhifadhi mazingira na kuboresha afya zao.

Joyce Komba mkazi wa Lusaka Halmashauri ya Mji Mbinga, alisema kuwa kampeni hiyo ya majiko sanifu itawasaidia kupunguza gharama za maisha kwani majiko hayo yanapika kwa haraka, kuokoa muda na kupunguza matumizi ya nishati nyingine zisizo rafiki kwa mazingira kama matumizi ya mkaa.
“Jiko hili la presha ni msaada mkubwa sana hasa kwa sisi watu wa kipato cha chini kama Mimi hapa naishi na mamaangu mzazi ambaye ni mdhaifu hivyo litanisaidia kuandaa chakula chake kwa wakati na matumizi ya mkaa yatapungua kwa kiasi kikubwa ” alisema Komba.
Rosemary Ramadhani mkazi Nyasa ameishauri Serikali kuongeza wigo wa mpango huu hadi vijijini, ili wananchi wote waweze kunufaika na fursa hii, hususani maeneo ambayo bado hutegemea kuni kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia.

Kwa upande wake, Afisa uhusiano huduma kwa wateja Lucia Renatus kutoka TANESCO Temeke ambaye ameambatana na maafisa wengine ameeleza kuwa mpango huo ni sehemu ya juhudi za shirika hilo kuhamasisha matumizi ya umeme kwa matumizi ya nyumbani, sambamba na kuchangia katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi kwa kupunguza ukataji wa miti ovyo.


