Na Mwandishi wetu,JamhuriMedia
Dar es Salaam

Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) limezindua mfumo wa kupokea taarifa za siri (Whistleblower portal) ambapo mfumo huo unaenda kurahisisha upokeaji wa taarifa kutoka kwa wananchi.

Amebainisha hayo Agosti 4,2025 Jijini Dar es Salaam,Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na huduma kwa wateja TANESCO, Irene Gowele amesema kwamba muda mrefu shirika hilo limekuwa likipata changamoto mbalimbali ambazo zinakwamisha utoaji wa huduma endelevu ya umeme ikiwemo wizi na uharibifu wa miundombinu ya umeme,pamoja na vitendo vya rushwa kutoka kwa baadhi ya watumishi wa shirika hilo.

“Mfumo huu mpya ni hatua muhimu ya kimageuzi katika utendaji kazi wa shirika la Ugavi wa umeme Nchini(TANESCO)ambao unaenda kudhibiti uhalifu, uwajibikaji na ulindaji wa taarifa dhidi ya vitisho na kuongeza uaminifu wa umma kwa shirika.”amesema Gowele

Nakuongeza kuwa” mtoa Taarifa ataelekezwa kwenye hatua stahiki huku taarifa hizo zikichukuliwa kwa siri kupitia mfumo huo hivyo sisi kama shirika tutashirikiana kwenye taarifa zote ambazo zitapelekwa na kutunzwa kwa siri na kushughulikiwa.”

Halikadhalika Shirika la Ugavi wa umeme Tanzania TANESCO limetoa wito kwa wananchi wote nchini kushiriki kikamilifu kwa kutumia mfumo huo ili kuweza kusaidia kulinda rasilimali na maslahi ya shirika na Taifa kwa ujumla.

“Kuna njia mbili ambazo zitatumika katika kuwasilisha taarifa hizo ambazo ni kupitia Tovuti ya TANESCO ambayo ni WWW.tanesco.co.tz ambapo unatakiwa kubonyeza kiungo cha (Whistleblowerportal) na utaweza kujaza fomu salama ya kutoa taarifa hiyo. ,kupiga simu ya bila malipo :Namba 180 kisha unabonyeza namba mbili na utaweza kuzungumza na watoa huduma wetu.

Aidha katika kuendelea na kampeni ya Shirika hilo ya nchi nzima ijulikanayo kama “lipa deni tukuhudumie” shirika linaendelea na kampeni hiyo katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati kwenye maeneo yao husika na kuondoa changamoto mbalimbali zinazojitokeza.