Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar es Salaam

TANZANIA Freight Forwarders Representation in Dubai @tanfordhub (TANFORD) imeandaa kongamano la siku mbili linalotarajia kufanyika Umoja wa Nchi za Kiarabu, Dubai ikiwa na lengo la kuinadi Tanzania katika masoko ya kimataifa na kufungua fursa kwa wafanya biashara wa Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa Habari,leo January 28,2026 Jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa TANFORD, Bw Hussein Jamal amesema kuwa kongamano hilo linaloitwa Tanzania Trade and Logistics Forum 2026 litafanyika Februari 13 na 14 na litawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya biashara na usafirishaji ili kufungua fursa zilizopo baina ya Tanzania na Dubai.

“Tumeandaa kongamano hili ili kuinadi nchi yetu kimataifa na kuifanya nchi yetu kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji afrika mashariki na kati na pia kusaidia kukuza matumizi ya bandari na miundombinu ya usafirishaji Tanzania kwa kukusanya mizigo katika masoko ya kimataifa kupita Tanzania,” alisema Bw Jamal.

Bw Jamal alisema kuwa kongamano hilo litasaidia kufungua fursa za masoko mapya ya bidhaa za kitanzania kuweza kufika kimataifa kwa kukutana na wateja mbalimbali ambao wanatarajiwa kuwepo kwenye kongamano hilo.

Alieleza, “TANFORD inasimama kama Daraja la kibiashara katai ya Tanzania na masoko ya kimataifa ili kuweza kuwasaidia watanzania wengi kuweza kuona fursa mbalimbali za biashara na usafirishaji zilizopo Dubai na pia kutangaza biashara zao huko.”

Hii ni fursa adhimu kwa wadau mbalimbali wanakaribishwa kwa sababu wanaenda kufungua fursa kwa mtu mmoja mmoja, kwa taifa na makampuni yanayofanya biashara ya usafirishaji kati ya Dubai na Tanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt Latifa Mohammed Khamis alisema kuwa ni muhimu kushiriki katika makongamano kama hayo kwani husaidia kukuza mahusiano bora baina ya wafanyabiashara wa hapa nchini na wa nje ya nchi.

“Rai yangu kwa wafanyabishara wa kitanzania ni muhimu kuudhuria kongamano hili kwani litafungua fursa ya kupata mashirikiano mbalimbali na wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali,” alieleza.

Naye rais wa Chama cha mawakala forodha Tanzania (TAFFA), Bw Edwin Urio amebainisha kuwa kushiriki katika kongamano hilo ni fursa ya kujikuza kibiashara, kujitagaza inakwenda kusaidia kukuza Uchumi wa Nchi.

“Sekta ya logistics na usafirishaji ndio sekta ambayo katika mwaka wa fedha uliopita 2024/2025 iliongoza katika kuingizia fedha za kigeni nchini na pia ni sekta ambayo ni uti wa mgongo wa Nchi yeyote ambayo inakua kiuchumi,”ame sema Bw Urio.

Pia aliwapongeza taasisi za serikali kwa kuungana katika jambo hilo ambalo linamanufaa katika kukuza Uchumi wan chi yetu.

Aidha Taasisi tofauti zinazotarajia kushiriki katika Kongamano hilo ni pamoja na TPA, TRA, DP WORLD, TAFFA, TANTRADE, TATOA, PORT MARINE CLEARING & FORWARDING, SILENT OCEAN & KILIMANJARO STAR CARGO na TPSF.