Na Mwandishi Wetu, Songea

WIZARA ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)Mkoa wa Ruvuma, imeanza ujenzi wa daraja la Mitomoni katika Mto Ruvuma lenye urefu wa mita 45 ambalo litaunganisha Wilaya ya Nyasa na Songea.


Meneja wa TANROADS Mkoani Ruvuma Mhandisi Saleh Juma alisema, watahakikisha wanakamilisha ujenzi wa daraja la Mitomoni haraka ili kuwezesha wananchi wa Wilaya hizo mbili wawe na uhakika wa usafiri na usafirishaji, kuchochea maendeleo na kupata huduma za kijamii kwa urahisi.

Mhandisi Saleh, ametaja gharama ya ujenzi wa daraja hilo ni Sh.bilioni 9.295 zilizotolewa na Benki ya Dunia na linalojengwa na Kampuni ya Kitanzania Ovans Contruction Ltd na ujenzi wake hadi umefikia asilimia 65.

Kwa mujibu wa Mhandisi Saleh,daraja hilo litaunganishwa na barabara ya Unyoni- Mpapa-Lipalamba-Mkenda na barabara ya Likuyufusi-Mkenda,na miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali katika Mkoa wa Ruvuma na linatarajiwa kumaliza changamoto ya mawasiliano kati ya Wilaya ya Nyasa, Songea na nchi jirani ya Msumbiji.

“Mpango wetu kuhakikisha daraja hili linakamilika mwezi wa tisa,tunaamini kazi iliyobaki tuna uwezo wa kukamilisha kama tulivyopanga na kumaliza kilio cha Wananchi wa Wilaya zote mbili ambao kwa muda mrefu wameteseka na kupata madhara makubwa kutokana na kuvuka kwenye mto Ruvuma”alisema Saleh.

Alisema,daraja hilo linahitajika kwa muda mrefu kwa sababu wananchi wa vijiji vya Mitomoni kwa upande wa Nyasa na Mkalawa Songea vijijini wakati wa masika, wanapata shida kutokana na mto Ruvuma kujaa maji mengi na kupelekea kukatika kwa mawasiliano,hivyo kushindwa kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo.

Alieleza kuwa,daraja hilo ni muhimu katika kurahisisha mawasiliano na litafungua fursa mbalimbali za maendeleo kwa wananchi na kukuza uchumi wa Wilaya ya Nyasa,Mbinga na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla na litaimarisha ulinzi wa nchi yetu.

Msimamizi wa mradi huo Mhandisi Pius Gwegendao alisema, wanahakikisha watamsimami mkandarasi ili aweze kujenga daraja hilo kwa kiwango na kukamilika kwa muda uliopangwa.

Mwakilishi wa Mkandarasi Mhandisi Emanuel Bilai amesema,mradi huo unahusisha ujenzi wa daraja lenyewe lenye urefu wa mita 45 na barabara unganishi ya lami za kilometa 8.

Alisema,hadi sasa kazi zilizofanyika ni ujenzi wa nguzo moja na nguzo ya pili ujenzi wake unaendelea na wameanza kujenga kuta ya katikati ya maji na litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kupitisha magari mawili kwa wakati mmoja na litakuwa na njia za watembea kwa miguu pande zote mbili.

Baadhi ya Wananchi wa vijiji vya Mitomoni Wilaya ya Nyasa na Milawa Wilayani Songea,wameishukuru Serikali kwa kuanza ujenzi wa daraja hilo ambalo litamaliza mateso ya kuvuka mto Ruvuma kwa kutumia usafiri wa Mitumbwi ambayo siyo salama.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkalawa Zuber Mohamed alisema,kuna ndugu zao wengi wamepoteza maisha baada ya kusombwa na maji walipokuwa wakijaribu kuvuka katika mto huo kipindi cha masika kutokana na kukosekana kwa daraja la uhahika.

Alisema,ujenzi wa daraja utaleta neema na manufaa makubwa kwao kwani litasaidia kuokoa maisha ya watu wengi,kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kuchochea uchumi wao.

Amewapongeza wasimamizi na mafundi wanaojenga daraja hilo kwa kazi nzuri wanayofanya,na ameiomba Serikali iwe karibu na Mkandarasi aweze kumaliza ujenzi wa mradi huo mapema kwani wanauhitaji mkubwa kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano ya usafiri.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mitomoni Ali Mpaiche alisema,watoto wanakatisha masomo wanapotaka kwenda shule upande wa pili na mama wajawazito wamejifungulia njiani na wengine kupoteza maisha kwa kushindwa kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa wakati.