Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema ziara yake nchini Belarus ambayo ni ya kwanza ya ngazi ya juu tokea nchi hizo zilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1996, imefungua mwanzo mpya wa ushirikiano katika maeneo ya kimkakati yenye manufaa kwa pande zote mbili.

Mhe. Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo mbele ya waandishi wa habari jijini Minsk, Belarus baada ya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Belarus, Mhe. Alexander Turchin Julai 22, 2025.

Alisema kusainiwa kwa Hati nne za Makubaliano (MoUs) katika maeneo ya mashauriano ya kisiasa, kilimo, elimu na biashara ambazo ni matokeo ya ziara hiyo ni ishara ya wazi kuwa nchi hizo zimeonesha utashi wa kisiasa wa kufanya kazi kwa pamoja kuendeleza rasilimali lukuki zilizobarikiwa na Mwenyezi Mungu.

Mhe. Waziri Mkuu alisema kufuatia Belarus kupiga hatua kubwa ya maendeleo katika sekta za kilimo, ellmu, TEHAMA, Afya, Nishati, viwanda na utalii, amemuomba mwenyeji wake azishawishi kampuni kubwa kwenye maeneo hayo kuja kuwekeza Tanzania.

Alisema mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania ni mazuri kufuatia maboresho mbalimbali yaliyofanywa na Serikali katika sera na sheria za uwekezaji, miundombinu na motisha za kikodi.

Alisema pia kuwa uhakika mkubwa wa soko unaotokana na eneo la kijigiografia ambalo Tanzania ipo na kuwa mwanachama wa Jumuiya za Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Eneo Huru la Biashara barani Afrika ambazo kwa pamoja zina idadi ya watu zaidi ya bilioni 1.6 inaifanya Tanzania kuwa sehemu sahihi ya uwekezaji.

Waziri Mkuu na ujumbe wake ambao unajumuisha Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais-Zanzibar, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Shariff Ali Shariff, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi, Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Mhe. Fredrick Kibuta na viongozi wengine waandamizi wa Serikali ulipata fursa ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza dawa na vifaa tiba na kiwanda cha kutengeneza matrekta na kujionea namna viwanda hivyo vinavyotumia teknolojia ya kisasa kuzalisha bidhaa bora.

Menejimenti za Viwanda hivyo zimekubali kushirikiana na Tanzania na zimeahidi kufanya ziara nchini hivi karibuni ili kujionea fursa za uwekezaji.