Na Mwandishi Maalum

Tanzania na Brazil zimeahidi kuendelea kushirikiana katika sekta za kimkakati zenye maslahi mapana kwa mataifa haya mawili ikiwemo Afya, Kilimo, biashara, uwekezaji, elimu na ulinzi na usalama.

Hayo yamebainishwa wakati wa mazungumzo baina ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe na Balozi wa Brazil nchini Mhe. Gustavo Martins Nogueira yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma Januari 29, 2026.

Viongozi hao wamejadili masuala kuhusu ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Brazil kwa kipindi cha miongo mitano iliyopita na kukubaliana kuendelea kuuimarisha ushirikiano huo na kuupeleka katika viwango vya juu ili kuwawezesha wananchi kunufaika nao.

Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Maghembe aliishukuru Serikali ya Brazil kwa kusaidia utekelezaji wa miradi ya zao la pamba ya Beyond Cotton na Cotton Victoria na kusistiza umuhimu wa kuibua miradi mingine zaidi.

“Miradi hii imejikita katika kuwasaidia wakulima wa pamba nchini kwa kuongeza thamani ya zao hilo na bidhaa zake pamoja na kuinua tija ya zao hilo kwa ujumla,” alisema Mhe. Maghembe.

Mhe. Maghembe aliiomba Serikali ya Brazil kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuchangia fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa kupambana na Ugonjwa wa Selimundu (Sickle Cell) nchini na kukamilisha majadiliano ya utekelezaji wa Mradi wa Afya ya Mama na Watoto wachanga- Zanzibar.

Vilevile, Mhe. Maghembe ameomba Brazil ishirikiane na Tanzania kuendeleza vipaji na kutoa uzoefu wao katika kuandaa mashindano mbalimbali ya michezo ili kujiandaa vyema na mandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) yanayotarajiwa kufanyika nchini mwaka 2027.

Kwa upande wake, Mhe. Nogueira ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwa mshirika wa karibu wa Brazil kwa maslahi ya pande zote.

Kadhalika, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kushiriki Mikutano mikubwa iliyofanyika Brazil ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alishiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kundi la Nchi 20 (G20) na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango alishiriki Mkutano wa Pili wa Brazil na Afrika kuhusu Usalama wa Chakula, Mapambano dhidi ya Njaa na Maendeleo Vijijini.

Tanzania na Brazil zinatarajia kuwa na majadiliano ya kisiasa yatakayofanyika mwezi Aprili 2026.