MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Chrispin Chalamila amesema Tanzania na Comoro zitaendelea kushirikiana katika maeneo matano ikiwemo utawala bora.

Chalamila amesema hayo Novemba 17, 2025 wakati alipotembelewa na ugeni kutoka nchini Comoro ulioongozwa na Rais wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  nchini Comoro.

Alisema ushirikiano kati ya Comoro na Tanzania ni wa kihistoria na umejengwa katika misingi ya kuheshimiana, kuunganishwa na tamaduni za kila nchi pamoja na kuwa na malengo ya pamoja ya amani na maendeleo.

“Kwa miaka kadhaa tumekuwa tukishuhudia maeneo kadhaa yakiimarika, hususan katika maeneo ya utawala bora na jitihada za kuzuia na kupambana na rushwa. Ushirikiano huu umekuwa ukifanyika kupitia ushirikiano wa kikanda pamoja ushauri wa Bodi ya Ushauri ya Umoja wa Afrika dhidi ya Rushwa (AUABC),” alisema Chalamila.

Alisema eneo jingine ni kubadilishana uzoefu kuhusu hatua za kupunguza rushwa, mbinu za utendekaji wa uhalifu uliojikita katika rushwa pamoja na mikakati ya kuelimisha umma na kuwashawishi kuepuka rushwa.

“Kushirikiana katika kuimarisha mifumo ya kitaifa ya kiuwadilifu, nyenzo za kutafuta vihatarishi vya uwepo wa rushwa na utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa na wadau ili kuziba mianya ya rushwa,” alisema.

Chalamila alisema eneo jingine la ushirikiano ni usalama na utekelezaji wa sheria kupitia juhudi za pamoja katika kuimarisha na kusimamia mipaka, hasa usalama wa Bahari ya Hindi pamoja na bandari, kwa kutumia fursa za miundombinu ya Tanzania na muunganiko na Comoro ili kuweka mipango ya kukuza biashara, utalii na uwekezaji.

Alisema eneo la nne ni kilimo, mafunzo na kujengeana uwezo kupitia programu mbalimbali za kubadilishana uzoefu na mafunzo kwa watumishi wa umma na katika utawala na uongozi.

“Kumekuwa na ushirikiano katika taratibu za utoaji wa ufadhili wa masomo na ushirikiano wa taasisi za elimu ya juu kati ya nchi hizi, na tutaendelea kuimarisha ushirikiano wetu kwa manufaa ya nchi zetu,” alisema Chalamila.

Alitaja eneo jingine la ushirikiano kuwa ni sekta ya afya na maendeleo ya jamii, kwa kupambana na kudhibiti magonjwa ya kuambukiza na kuimarisha mifumo ya afya ya umma kwa ujumla.

Chalamila alisema kwa sasa taasisi hiyo ina jumla ya ofisi 145 ambazo ni makao makuu, 28 za mikoa, 111 za wilaya pamoja na vituo maalumu sita katika maeneo yenye mzunguko mkubwa wa fedha na mipakani.

Kwa upande wake, Rais wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Comoro, Fahamoue Youssouf, alisema ujio wao unaonyesha uwazi wa taasisi hizo kupitia suala la kubadilishana uwezo juu ya mapambano ya rushwa kikanda na Afrika kwa ujumla.

Alisema ushirikiano huo utafungua njia ya ushirikiano endelevu, iwe kupitia mafunzo, uzoefu au kuanzishwa kwa mifumo rasmi kati ya nchi hizo.

Aliongeza kuwa matarajio yao ni kuhakikisha azimio la pamoja linatimia, kwa kuwa watajifunza kutokana na uzoefu na matarajio yenye matumaini ya ushirikiano kati ya taasisi hizo kwa lengo la kuimarisha utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa.         

.