Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
UBALOZI wa Finland nchini umesema utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuongeza umuhimu wa matumizi ya mifumo ya kidijiti kwa vijana wajasiriamali ili kuboresha huduma za umma na ujasiriamali.
Balozi wa Finland nchini, Theresa Zitting alisema hayo jana Dar es Salaam kwenye warsha ya wiki ya Nordiki 2025 yenye lengo la kukuza ubunifu endelevu na matumizi ya kidijiti katika ujasiriamali kwa vijana.
Alisema Mwaka huu, wameangazia uendelevu, mabadiliko ya kidijiti na ubunifu kwa wanafunzi, wajasiriamali, washauri wa biashara na waendelezaji wa mazingira ya ubunifu ili kuona umuhimu wa mawasiliano katika kuongeza thamani ya ubunifu kwa vijana wajasiriamali.
Alieleza kuwa warsha hiyo imeandaliwa kwa vijana wajasiriamali kwa sababu ya kukua kwa kasi kwa matumizi ya kidijiti yanayobadilisha namna ya kuishi,kufanya kazi na kuwasiliana.
