Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania inaendelea kupiga hatua muhimu katika safari yake ya kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa, teknolojia na rasilimali za ndani.
Taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Bw. Shaaban Kissu imesema Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo wakati akizindua Kiwanda cha Majaribio cha Uchenjuaji wa Madini ya Urani kilichopo Wilaya ya Namtumbo, kinachomilikiwa na kampuni ya Mantra Tanzania Limited.
“Tunataka Watanzania waone manufaa ya moja kwa moja kutoka mradi huu. Ni wajibu wetu kuhakikisha ajira zinatolewa kwa wananchi hususan wa maeneo yanayozunguka mradi na kwamba mapato yake yanaimarisha huduma za kijamii,” alisema Rais Dkt. Samia.

Aidha, Rais Dkt. Samia amesema Serikali inatambua uwekezaji huo kuwa wa kimkakati unaoweza kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa taifa na wananchi na kuongeza kuwa urani ni rasilimali yenye uwezo wa kuimarisha uchumi, kuzalisha ajira na kuongeza mapato ya nchi.
“Kiwanda hiki cha majaribio ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati yetu ya kuhakikisha tunatumia madini haya kwa manufaa ya Watanzania wote kwa kuzingatia usalama wa kiafya, kimazingira, na kufuata viwango vya kimataifa,” alisema Rais Dkt. Samia.
Aliongeza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zenye akiba kubwa ya madini ya urani, ikiwemo hifadhi ya tani 60,000 ya madini hayo katika eneo la Mto Mkuju pekee, jambo linaloliweka Taifa katika rekodi nzuri ya umiliki wa rasilimali hii.
Halikadhalika, Rais Dkt. Samia amesema utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 wa kuifanya Tanzania kuwa taifa lenye viwanda na uchumi wa kati wa juu unaojitegemea, na hivyo kuiweka miongoni mwa nchi wachangiaji wakubwa 10 duniani wa malighafi muhimu ya nishati safi ya nyuklia.

Akifafanua manufaa ya kiuchumi, Rais Dkt. Samia amesema uwekezaji wa mradi huo unaokadiriwa kufikia Dola za Marekani Bilioni 1.2, utazalisha zaidi ya ajira 8,700 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, huku Serikali ikinufaika na mapato ya takribani Dola Bilioni 1 kupitia kodi, mirabaha na gawio kutokana na umiliki wake wa asilimia 20.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia ameitaka kampuni ya Mantra Tanzania Limited kutekeleza mradi huo kwa kuzingatia wajibu wa kijamii na ushirikishwaji wa Watanzania, huku akizitaka Wizara na Taasisi zinazohusika na usimamizi wa mazingira kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uendelevu na usalama wa mazingira.
Vilevile, Rais Dkt. Samia alibainisha kuwa Serikali itaendelea kujifunza kupitia uzoefu wa nchi rafiki kama Jamhuri ya Namibia, ambayo imekuwa ikichimba urani kwa muda mrefu, ili kuhakikisha uendelevu wa mradi huo unakwenda sambamba na ulinzi wa mazingira.



